22: Urithi

Kasri la Kifalme Mjini Beijing

Katikati ya mji wa Beijing kuna jamii kubwa ya majumba ya zamani ya adhama na fahari, hilo ndio kasri la kifalme lililo maarufu sana duniani, na vilevile ni kasri pekee lililojengwa kwa mbao tupu. Kasri hilo liliorodheshwa na UNESCO katika kumbukumbu za urithi wa utamaduni wa Dunia mwaka 1987.

Kasri la kifalme lililopo Beijing lilijengwa kwa amri ya mfalme wa pili wa Enzi ya Ming, Zhu Li, mswaka 1406, na ujenzi wake ulitumia miaka 14. kabla ya enzi ya mwisho nchini China yaani Enzi ya Ming kumalizika mwaka 1911, katika muda wa miaka 500 hivi, jumla ya wafalme 24 walikaa katika kasri hilo kushughulika na mambo ya taifa. Ni nadra kuona kasri kama hilo duniani lingeweza kulingana ama katika ukubwa wake, au katika mtindo mzuri na wa fahari wa majumba au katika samani na vyombo vya mapambo. Eneo la kasri ni zaidi ya mita za mraba laki 7 na elfu 20, urefu kutoka kaskazini hadi kusini ni mita 1,000, na upana kutoka magharibi hadi mashariki ni mita 800, pembezoni unazungukwa kwa ukuta na nje ya ukuta ni handaki la maji lenye upana wa mita 50. Kasri hilo lilijengwa kwa kufuata moja kwa moja utaratibu na dhana za kimwinyi, yaani ama katika mpangilio wa majumba au katika ukubwa wa ujenzi, au katika mtindo na rangi ya majumba au katika samani na vyombo vya mapambo yote yameonesha sana utukufu na madaraka makubwa ya mwisho ya mfalme. Miongoni mwa majumba yote ya kasri hilo, zinazovutia zaidi ni kumbi tatu kubwa, yaani ukumbi wa Taihe, ukumbi wa Zhonghe na ukumbi wa Baohe, hizo kumbi ni mahali pa kufanyia sherehe kubwa. Kati ya kumbi hizo tatu, ukumbi wa Taihe ni kitovu cha majumba yote ya kasri hilo, kiti cha enzi kiko ndani ya ukumbi huo. Huu ni ukumbi unaoonekana wenye adhama kubwa, ambao umejengwa upande wa kaskazini katika uwanja wenye eneo la mita za mraba elfu 30 kwenye jukwaa lenye matabaka matatu na kimo cha mita 8, kimo cha ukumbi huo ni mita 40, hilo ni jumba refu kabisa kuliko majumba yote mengine katika kasri. Katika utamaduni wa China, dragoni anamaanisha madaraka ya mfalme, mfalme ndiye "dragoni halisi na mwana wa mungu", kutokana na dhana hiyo ukumbi huo umepambwa kwa dragoni karibu elfu 13. Ujenzi wa kasri pia umedokezea masimulizi mengi na umetumia ujuzi mkubwa. Kwa mfano, kasri hilo lina jumla ya vyumba 9,999 na nusu. Hii inatokana na wazo ambalo wahenga wa China waliamini kuwa peponi kuna vyumba 10,000, kwa kujizuia mfalme alijenga idadi ya vyumba kasoro nusu ya chumba chini ya idadi ya vyumba peponi. Ndani ya bustani, kuna jiwe moja kubwa ambalo juu yake zilichongwa sanamu za mazimwi na vibwengo, kwani katika bustani hiyo kuna ukumbi mmoja ambao ulisemekana kwamba aliwahi kukaa mungu mmoja, siku moja ukumbi huo ulikumbwa na ajali ya moto, mungu huyo aliongoza wazimamoto waliokuwa samaki na majoka kuuzima, baadaye aliweka jiwe hilo kama ni kumbukumbu. Kadhalika, kwa sababu majumba yote yamejengwa kwa mbao tupu, ili kuzuia ajali ya moto usienee kwenye majumba halisi, mafundi walitumia akili nyhingi, wakajenga safu nne za nyumba ambazo kwa wajihi ni nyumba lakini kwa ndani ni mawe tupu ili kuzuia ajali isienee zaidi. Ndani ya kila ua wa jumba iliwekwa mitungi mikubwa ya maji jumla 308, ndani ya mitungi hiyo ya shaba, maji yalikuwa tayari wakati wote kwa kuzima moto, na katika majira ya baridi moto uliwashwa chini ya mitungi ili maji yasigande. Kutokana na rekodi ya historia, ujenzi wa kasri ulitumia wafanyakazi na mafundi laki moja, vifaa vya ujenzi vilitoka kutoka pande mbalimbali nchini China ikiwa ni pamoja na mko wa Yunnan, mkoa uliopo kusini magharibi mwa China ulio mbali kwa kilomita elfu kadhaa kutoka Beijing. Ndani ya kasri hilo vinahifadhiwa vitu vyenye thamani kubwa vya kumbukumbu za utamaduni zaidi ya milioni ambavyo ni kiasicha sehemu moja kwa sita ya vitu vyote vya utamaduni nchini China, na miongoni mwa vitu hivyo baadhi ni johari za kitaifa. Ili kuhifadhi vema vitu hivyo katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, serikali ya China ilijenga bahari yenye vyumba zaidi ya 100 chini ya ardhi. Kasri hilo la kifalme ni alama ya utamaduni mkukbwa wa China. Wataalamu wa China na nchi za nje wanaona kuwa usanifu na ujenzi wa kasri hilo ni kazi bora isiyo kifani, ni maonesho ya utamaduni mkubwa wa China na ni uhodari mkubwa wa mafundi waliokuwepo kabla ya miaka 500 iliyopita. Hadi leo kasri hilo limekuwa na historia ya miaka zaidi ya 580, majengo yake yamedumu kwa miaka mingi, zaidi ya hayo, katika miaka ya karibuni watalii wanaongezeka haraka hadi karibu milioni 10 kwa mwaka. Ili kutunza vema kasri hilo serikali ya China kuanzia mwaka jana ilianza kukarabati kasri hilo, na ukarabati huo utaendelea kwa miaka 20.

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14