22: Urithi

Hekalu la Confucius

Confucius alikuwa mwanafalsafa, mwanasiasa na mwelimishaji mkubwa katika zama za Spring na Autumn yaani toka mwaka 770 K.K. hadi 475 K.K. nchini China.

Hekalu la Confucius liko mjini Qufu mkoani Shandong, mashariki mwa China. Mwaka 478 K.K., mwaka wa pili baada ya Confucius kufariki, mfalme wa Dola la Lu aligeuza makazi ya Confucius kuwa hekalu, na aliweka vitu alivyotumia Confucius ndani ya hekalu kama nguo, kofia na baadhi ya vyombo vya kutolea sadaka. Mfalme huyo kila mwaka alikwenda huko kufanya tambiko. Tokea hapo na kuendelea, kwa miaka zaidi ya elfu mbili, utamaduni ulioanzishwa na Confucius umezidi kuota mizizi katika ardhi ya utamaduni wa Kichina. Wafalme wa kila enzi hawakuksahau kujenga zaidi na kulifanya hekalu hilo kuwa lenye fungu kubwa la majengo. Katika karne ya 18 mfalme wa Enzi ya Qing aliamrisha kuongeza majengo mengi kupita enzi zote akatupatia hekalu la leo.

Hekalu la Confucius lina urefu wa mita zaidi ya 1,000 kutoka kusini hadi kaskazini, eneo lake ni mita za mraba karibu laki moja, lina vyumba 500. Ujenzi wa hekalu hili ulitumia kiwango cha juu kabisa cha ufundi katika jamii ya umwinyi nchini China kwa kiwango cha ujenzi wa kasri ya kifalme. Majengo yake muhimu yanapangwa kwenye mstari wa katikati, na pande mbili za mstari huo, ni majengo mawili mawili ya kufanana na kukabiliana. Mpangilio huo wa ulinganifu wa majengo umeongeza utukufu na adhama. Ujenzi wa hekalu la Confucius ulitumia sana tarakimu 9. Mathalan, kuna nyua tisa mbele ya kumbi tisa, kati ya kumbi hizo ukumbi mkuu kwa jina la Dacheng una nafasi ya vyumba tisa. Tisa ni namba kubwa kabisa miongoni mwa tarakimu moja. Katika jamii ya umwinyi nchini China "tisa" iliruhusiwa tu kutumika kwa ajili ya mfalme, hasa katika ujenzi, yeyote mwingine akitumia "tisa" atakatwa kichwa, lakini kwa hekalu la Confucius ilikuwa vingine. Kabla ya kufikia ukumbi mkuu wa Dacheng kuna milango mitano, ambayo kisheria milango mitano ya kuingilia ndani haikuruhusiwa kutumika katika ujenzi ila tu kasri ya kifalme. Lakini hekalu la Confucius lilijengwa kwa milango mitano, hii imeonesha heshima kubwa kwa Conficius sawa na mfalme.

Ukumbi mkuu wa Dacheng ni mahali hasa pa kufanyia tambiko kwa Confucius. Ukumbi huo una urefu wa kwenda juu mita 30 na upana kutoka mashariki hadi kaskazini ni zaidi ya mita 50, paa yake imeezekwa kwa vigae vya kauri ya njano, kwenye upenu wa ukumbi huo kuna nguzo 10 za mawe, ambazo juu ya kila nguzo wamechongwa dragoni waliouzungushia nguzo mawinguni. Kila nguzo ina urefu wa mita 6 na kipenyo karibu mita moja. Juu ya nguzo hizo kumi hakuna dragoni hata moja anayefanana na mwingine, chini y amwanga wa jua kwa mbali dragoni wanaonekana kama wa kweli, ni michongo yenye thamani kubwa katika sanaa ya michongo ya kale ya China, hata limeshinda nguzo ndani ya kasri ya kifalme mjini Beijing. Inasemekana kwamba kila mfalme alipokwenda huko kufanya tambiko, nguzo hizo zilifungwa kwa kitambaa cha hariri nyekundu ili mfalme asikasirike iwapo akigundua kuwa kuna dragoni kwenye nguzo.

Makazi ya Confucius ni nyumba za kuishi Confucius na vizazi wake.

Makazi ya Confucius yalijengwa katika karne ya 12 hadi 13, eneo lake ni mita za mraba 50,000, vyumba 500. Ndani ya makazi kuna kumbukumbu nyingi za historia, mapambo ya nguo na vyombo vya kazi.

Msitu wa Confucius ni sehemu ya makaburi ya Confucius na vizazi wake. Ni makaburi yenye maeneo makubwa ya yenye historia ndefu kabisa duniani. Makaburi hayo yalikuwa yanaongezeka katika muda wa miaka 2500, eneo lake ni kilomita mbili za mraba, kuna makaburi ya watu wenye jina la ukoo Confucius zaidi ya laki moja.

Makaburi ya Confucius na vizazi wake yana tahamani kubwa kwa ajili ya utafiti wa mambo ya kale kuhusu siasa, uchumi, utamaduni na mila ya mazishi.

Katika sehemu za Hekalu, makazi na makaburi kuna miti ya miaka mingi 17000, ambayo ni kama mashahidi wa historia ya maendeleo ya sehemu hizo tatu.

Mwaka 1994 UNESCO imeingiza sehemu tatu za hekalu, makazi na makaburi ya Confucius katika urithi wa dunia.

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14