Scotland yasema haitapiga kura za maoni kuhusu kujitenga na Uingereza kabla ya Brexit
Waziri mkuu wa serikali ya Scotland na kiongozi wa chama tawala cha SNP Bibi Nicola Sturgeon, amesema serikali ya Scotland itapanga upya ajenda ya kupiga kura za pili za maoni kuhusu kujitenga na Uingereza, na haitapiga kura hizo kabla ya Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya.
Bibi Sturgeon amesema, matokeo ya uchaguzi mkuu wa Uingereza yameonesha udhaifu wa serikali ya Uingereza, hali ambayo inaweza kuifanya serikali ya Uingereza ilegeze msimamo kwenye mazungumzo ya kujitoa Umoja wa Ulaya, na pia imepunguza uwezekano kwa Uingereza kubaki kwenye soko la pamoja la Ulaya.
Ameongeza kuwa serikali ya Scotland itaweka upya mpango wa kupiga kura za maoni kuhusu kujitenga na Uingereza, kwa kuzingatia mambo ya kujitoa Umoja wa Ulaya.
Na nchini Uingereza wiki hii Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema raia wa Umoja wa Ulaya wanaoishi nchini mwake, wanaendelea kuwa na haki sawa na raia wa nchi hiyo.
May amewaambia viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya jijini Brussels kuwa, hakuna atakayebaguliwa hata baada ya nchi yake kuanza kujiondoa katika Umoja huo.
Amesisitiza kuwa raia wa mataifa mengine ambao wameishi nchini Uingereza kwa zaidi ya miaka mitano, watakuwa na haki ya kupata huduma ya afya, elimu na haki zingine muhimu nchini humo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |