Rwanda yashutumiwa kwa kuwaua 37 wenye makosa madogo
Vikosi vya usalama nchini Rwanda vimeshutumiwa kwa kuwaua takriban watu 37 wanaoshukiwa kufanya makosa madogo madogo tangu mwezi Aprili 2016 kulingana na ripoti ya Human Rights Watch HRW.
Ripoti hiyo inasema kuwa hatua hiyo inaonekana kuwa mpango wa makusudi kuwaua washukiwa wa wizi.
Mashahidi wameambia HRW kwamba hatma ya mtu mmoja anayetuhumiwa kuiba ng'ombe iliamuliwa katika mkutano wa kijamii.
Wengine waliambia HRW kwamba wengine waliouawa walituhumiwa kwa kuiba ndizi, pikipiki, kuingiza bangi kupitia mpaka wa taifa hilo na DR Congo ama hata kutumia neti haramu za uvuvi.
Maafisa wa Rwanda walikana kwa HRW kwamba mauaji ya kiholela yalifanyika.
HRW ilisema mwaka 2015 kwamba pia ilikuwa imenakili kukamatwa maelfu ya watu wakiwemo watoto wa kurandaranda mitaani pamoja na makahaba.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |