Serikali ya Nigeria imesema wengi wa watoto 110 waliotekwa na wapiganaji wa Kiislami kutoka mji wa Dapchi mwezi uliopita wamerejeshwa.
Wizara ya habari nchini Nigeria imesema wanafunzi 101 kati ya 110 walirudishwa mapema hii leo baada ya juhudi za kichinichini za hapo awali.'
Hata hivyo, taarifa hiyo haikuzingatia idadi ya wasichana waliofariki na imesema hakuna kikombozi kilicholipwa kwa wapiganaji hao.
Taarifa hata hivyo zinadokeza kwamba wasichana takriban watano walifariki wakiwa mateka, na msichana mmoja ambaye ni Mkristo bado hajasalimishwa na anaendelea kushikiliwa mateka.
Babake msichana huyo amesema anaendelea kuzuiliwa na wanamgambo hao kwa sababu amekataa kuslimu. Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, amesema ana furaha kwamba msichana huyo hakuikana dini yake.
Wasichana hao walitekwa walipokuwa shuleni siku ya Jumatatu jioni, tarehe 19 , na kundi la waasi ambao walikuwa wameuvamia mji wa Dapchi.
Hapo awali, ilidaiwa kwamba wasichana wengi walikuwa wametoroka na hakuna aliyekuwa ametekwa.
Lakini wiki moja baadaye, viongozi walikiri walikuwa wametekwa na waasi wa Kiislamu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |