Nchi za Afrika zasaini makubaliano ya kuanzisha eneo la soko huria
Nchi 44 za Afrika zimesaini makubaliano ya kuanzisha eneo la biashara huria, katika mkutano wa kilele wa 10 usio wa kawaida uliofanyika mjini Kigali.
Makubaliano hayo yalisainiwa na wakuu 19 wa nchi na serikali waliohudhuria mkutano huo, na kuyakabidhi makubaliano hayo kwa mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Mahamat.
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Rwanda Paul Kagame, amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hitimisho la mpango uliwekwa miaka 40 iliyopita kwenye mpango wa utekelezaji wa Lagos uliopitishwa mwaka 1980.
Makubaliano hayo yana lengo la kuziunganisha nchi zote 55 wanachama wa umoja wa Afrika na kuwa soko moja huria la huduma na bidhaa.
Rais Kagame amesema mbali na kuimarisha biashara kati ya nchi wanachama, eneo hilo pia linatarajiwa kuimarisha uhusiano na wadau wengine.
Kamati ya umoja wa mataifa inayoshughulikia uchumi wa Afrika imesema inatarajia kuwa eneo hilo litaongeza biashara barani Afrika kwa asilimia 53.2 kutokana na kufuta ushuru.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |