Zambia yakanusha ripoti za mlipuko wa Ebola mjini Lusaka
Mamlaka za Afya nchini Zambia wiki hii zimekanusha ripoti kwamba nchi hiyo imerekodi mgonjwa wa kwanza wa Ebola.
Ripoti zilizotolewa na vyombo vya habari vya nchi hiyo zinasema Zambia Jumatatu ilirekodi mgonjwa wa kwanza wa Ebola kufuatia kulazwa kwa mgonjwa mwenye umri wa miaka 41 katika hospitali ya Levy Mwanawasa, mjini Lusaka.
Akikanusha ripoti hizo waziri wa Zambia amesema mgonjwa aliyewekewa karantini katika hospitali hakuwa mgonjwa wa Ebola isipokuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa septicemia ambayo ni maambukizi ya bakteria kwenye damu. Amesema vipimo vya maabara vimeonesha kuwa mgonjwa hakuwa na virusi vya Ebola, na kuongeza kuwa hakuna haja ya kuogopa.
Amesema serikali imeongeza hatua za uangalizi kwenye maeneo ya mpaka na DRC, na kwamba timu ya watu sita ya uangalizi imewekwa kwenye wilaya zote zinazopakana na DRC.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |