IMO laandikisha zaidi ya watu 32,000 waliokosa makazi nchini Sudan Kusini
Shirika la Uhamiaji la Kimataifa IMO limesema limekamilisha zoezi la uandikishaji kwa kuchukua alama za vidole ambalo limethibitisha kuwa jumla ya watu 32,113 waliokosa makazi wanaishi kwenye maeneo mawili ya kulinda raia ya Juba, nchini Sudan Kusini.
Kwenye taarifa yake shirika hilo limesema idadi ya walioandikishwa inaonesha kushuka kwa asilimia 18 kutoka idadi ya awali ya mwaka 2016. Idadi hiyo imeshuka kutokana na kuhamisha watu 3,379 kutoka eneo namba 3 na kupelekwa kwenye eneo la muda la Mangateen kufuatia mvutano kati ya jamii.
Kulingana na shirika hilo eneo namba moja kati ya hayo mawili lina watu wachache wapatao 7,515 huku eneo namba 3 likisaliwa na watu elfu 24, 598 waishio huko.
Mkuu wa Operesheni wa IMO nchini Sudan Kusini, Tya Maskun amesema mafanikio ya zoezi hili yanategemea zaidi ushirikiano wa karibu kati ya washirika mbalimbali wa mashirika ya misaada ya kibinadamu na Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |