Watu 19 wauawa kwenye maandamano Sudan
Serikali ya Sudan inasema watu 19 wamepoteza maisha katika maandamano yanayoendelea katika miji mbalimbali nchini humo kulalamikia kupanda kwa bei ya mkate.
Maandamano yaliyoanza kwa amani, yamegeuka na kuwa makabiliano makali kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama hasa jijini Khartoum.
Licha ya malalamiko ya kupanda kwa bei ya mkata, waandamanaji pia wanamtaka rais Omar Al Bashir ajiuzulu.
Waziri wa habari na msemaji wa serikali ya Sudan Bw Bushara Gumaa Aro amesema kati ya watu 19 waliouawa, kuna wanajeshi wawili. Wanajeshi 187 na raia 219 wamejeruhiwa. Ameshutumu uingiliaji kutoka nje kwenye tukio hilo, ambao amesema wanatia chumvi kuhusu idadi ya watu waliouawa.
Katika wiki iliyopita maeneo mengi ya Sudan ukiwemo mji mkuu Khartoum, yameshuhudia maandamano makubwa ya kupinga kuzorota kwa uchumi na kuongezeka kwa bei ya bidhaa za msingi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |