Venezuela yakatisha uhusiano wa kibalozi na kisiasa na Marekani
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema nchi yake imeamua kukatisha kabisa uhusiano wa kibalozi na kisiasa na Marekani kutokana na nchi hiyo kupanga mara kwa mara mapinduzi ya kisiasa ndani ya Venezuela.
Rais Maduro amesaini waraka husika na kuwataka wanadiplomasia wa Marekani nchini Venezuela waondoke ndani ya saa 72.
Amesema kitendo cha rais Donald Trump wa Marekani kumwunga mkono mwanasiasa wa chama cha upinzani ambaye ni spika wa Bunge Bw. Juan Guaido kuwa "rais wa muda" ni hatua isiyo na busara.
Mzozo wa kisiasa nchini Venezuela umechukua sura mpya baada ya Marekani kumtambua rasmi kiongozi wa upinzani Juan Guaidó kama rais wa mpito.
Mataifa saba ya Amerika Kusini Brazil, Colombia, Chile, Peru, Ecuador, Argentina na Paraguay wametangaza kumuunga mkono Guaidó kama rais halali.
Canada pia imetangaza kumuunga mkono huku Umoja wa Ulaya (EU) wakitaka uchaguzi mpya ufanyike.
Lakini Mexico, Bolivia na Cuba zimetangaza kuendelea kumuunga mkono Maduro.
Maduro aliapishwa kuendelea na awamu ya pili ya urais mapema mwezi huu baada ya uchaguzi wa mwezi Mei mwaka jana ambao ulisusiwa na upinzani na kutuhumiwa kuwa na kasoro kadhaa ikiwemo wizi wa kura.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |