China yaitaka Canada kumwachia huru Bibi Meng Wanzhou mara moja
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bibi Hua Chunying amesema, China inataka Canada kumwachia huru Bibi Meng Wanzhou mara moja, na kuhakikisha haki na maslahi yake halali.
Pia amesema China inaitaka Marekani kurekebisha makosa yake, kuondoa amri ya kumkamata Bibi Meng Wanzhou, na kutoitaka Canada kumpeleka rasmi nchini Marekani.
Bibi Hua Chunying amesema, China kwa mara nyingi imeeleza msimamo wake kuhusu tukio hilo, na kusema hii siyo kesi ya kawaida ya kisheria.
Amesema Canada inatumia vibaya mkataba wa kubadilishana wahalifu kati yake na Marekani, na imekiuka usalama, haki na maslahi halali ya raia wa China.
Awali China imesema mpango wa Marekani kutaka Bibi Meng Wenzhou kusafirishwa kutoka Canada kwenda Marekani hauendani na sheria za kimataifa na sio halali.
Bibi Hua Chunying amesema ombi la Marekani kutaka Bibi Meng asafirishwe kutoka Canada linahusiana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.
Kampuni ya Huawei imesema mara nyingi kuwa inafuata sheria zote na kanuni za nchi inakofanya kazi.
China inapinga Marekani kuchukua hatua za upande mmoja dhidi ya Iran nje ya mpango wa Umoja wa mataifa, kitendo ambacho ni kinyume na sheria za kimataifa na kinapingwa na dunia, ikiwa ni pamoja na washirika wa Marekani. Canada pia inapinga vitendo hivyo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |