Mjumbe wa China atoa wito wa ufumbuzi wa kisiasa wa msukosuko wa Venezuela
Mjumbe wa China ametoa wito wa ufumbuzi wa kisiasa wa msukosuko wa Venezuela na kutaka vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi hiyo viondolewe.
Mjumbe wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Ma Zhaoxu ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kuwa, China inatoa wito kwa serikali ya Venezuela na upinzani kutafuta ufumbuzi wa kisiasa kupitia mazungumzo na mashauriano chini ya mfumo wa katiba na sheria.
Amesema China inaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya Venezuela katika kulinda mamlaka, uhuru na utulivu wa nchi na kusisitiza kuwa mambo ya Venezuela yanapaswa kuamuliwa na watu wa Venezuela wenyewe. Ameongeza kuwa China inapinga uingiliaji wa nje katika mambo ya ndani ya Venezuela, inapinga uingiliaji wa kijeshi nchini humo na pia inapinga matumizi ya visingizio vya kibinadamu kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa.
Balozi huyo pia amezitaka nchi husika ziondoe vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Venezuela, kwa kuwa vikwazo havisaidii utatuzi wa mgogoro, na havitaleta amani nchini humo.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |