Ethiopia yasema pande mbili za Sudan zimekubali kushikilia makubaliano ya awali
Wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imesema, pande mbili za nchini Sudan zimekubali kushikilia makubaliano ya awali kuhusu miundo, mamlaka na majukumu ya serikali ya mpito.
Wizara hiyo imetoa taarifa ikisema, maafikiano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo kati ya mwakilishi maalum wa Ethiopia kwenye suala la Sudan Mohamoud Dirir na pande mbalimbali za Sudan, kwa lengo la kutafuta utatuzi wa hali ya kisiasa nchini humo kwa njia ya amani.
Wizara hiyo pia imesema, ikiwa ni sehemu ya maafikiano hayo, mazungumzo yataanza upya hivi karibuni ili kutatua migongano inayobaki, ikiwemo baraza la kiraia na masuala mengine husika.
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutokomeza vurugu nchini Sudan na kurejesha mazungumzo kati ya waandamanaji na Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC).
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema, wanafuatilia hali inavyoendelea nchini Sudan, na kutumai mazungumzo ya kisiasa yataanza tena. Ameongeza kuwa, mamlaka husika zinapaswa kuacha kukamata na kuzuia watu ambao wana nafasi kubwa katika mazungumzo hayo, na pia kurejesha huduma za mtandao wa internet na njia nyingine za mawasiliano.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |