Kiwango cha umaskini kupungua- Kwa mujibu wa bajeti mpya.
Kiwango cha umaskini kimeelezwa kupungua katika maeneo yote (Mijini na Vijijini), ambapo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango amesema, umaskini umepungua Mijini kutoka 21.7% hadi 15.8% na maeneo ya vijijini umepungua kutoka 33.3% hadi 31.3%".
Hayo yalisemwa siku ya Alhamisi Juni 11, 2020 na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, wakati akisoma bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/20 bungeni Dodoma.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, hadi Aprili mwaka huu, jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa nchini. Ongezeko hili la viwanda limeongeza utoshelevu wa bidhaa nchini, mathalani uwezo wa uzalishaji wa Saruji umeongezeka kutoka Tani Mil 4.7 2015 hadi Tani Mil 9. 1 mwaka 2019.
Vile vile, hadi Aprili mwaka huu, serikali imeboresha miundombinu ya huduma za afya kwa kujenga Zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Halmashauri 71, za Rufaa 10, za Kanda 3, kuongezeka kwa Bajeti ya vifaa na dawa kutoka Bil 31, 2015 hadi Bil 269 2019.
Waziri Mpango alisema kwamba, kufikia Aprili mwaka huu, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dolla za Marekani Bil 5.3. Kiasi hiki kinatosheleza mahitaji ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6 ukilinganisha na Dolla Bil 4.4 cha mwaka 2015.
Swala kuu lingine ni ukuaji wa Pato la Taifa, ambao unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya 6.9% na kufikia 5.5% mwaka huu, ikilinganishwa na 7% mwaka 2019. Hii ni kutokana na mvua nyingi ambazo zimeharibu miundombinu ya usafirishaji nchini na athari za ugonjwa wa virusi vya corona.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |