Mkurugenzi wa shirika la WHO ukanda wa Afrika Matshidiso Moeti amesema virusi vimesambaa zaidi ya maeneo ya miji mikuu na kuwa upungufu wa vipimo na vifaa vingine ni changamoto katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Mpaka sasa Afrika limekuwa bara lililo na maambukizi ya chini ya virusi vya corona.
Afrika Kusini ilikuwa na zaidi ya robo ya wagonjwa walioripotiwa na ilishuhudia idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vilivyothibitishwa eneo la Eastern Cape na Western Cape. Haya ni kwa mujibu wa Dkt Moeti akitoa ripoti kwenye mkutano wa WHO makao makuu, Geneva.
Aliongeza kuwa Jimbo la Western Cape lilikuwa sawa na mwenendo wa mlipuko wa virusi Ulaya na Marekani.
Nchi hiyo ina moja kati ya mifumo mizuri ya kiafya barani Afrika, lakini kuna hofu kuwa ongezeko la maambukizi litafanya mfumo huo uzidiwe.
Serikali ya Afrika Kusini imesifiwa kwa kuchukua hatua mapema za kuweka masharti ya kutotoka nje, lakini kupunguza makali ya masharti hayo mwezi Juni kumehusishwa na ongezeko la maambukizi nchini humo.
Kwa ujumla zaidi ya watu milioni 7.3 wameabukizwa na zaidi ya watu 416,000 wamepoteza maisha duniani.
Dkt Moeti amesema Afrika ina watu 200,000 walioambukizwa na vifo 5,000, huku nchi 10 zikiwa na 75% ya maambukizi.
Dkt Moeti anasema kwamba ingawa idadi hii ya walioambukiwa Afrika ni chini ya 3% ya maambukizi duniani, ni wazi kuwa janga hili linashika kasi.
Ametahadharisha uwezekano wa ongezeko la maambukizi siku za usoni.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |