KENYA: MAHABUSU 10,000 WAACHILIWA KIPINDI CHA CORONA.
Zaidi ya wafungwa 10,000 wenye makosa madogo wameachiliwa huru kutoka magereza mbalimbali nchini Kenya, wakati wa janga la Covid-19. Haya yamethibitishwa na kamishna wa Magereza Wycliffe Ogallo.
Hatua hii inapelekea magereza 129 kote nchini kusalia na wafungwa 42,596. Kuachiliwa huru kwa wafungwa hao ni sehemu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Baraza la Kitaifa la Kusimamia Haki (NCAJ) kwa lengo la kupunguza misongamano katika magereza nchini Kenya. Waliochiliwa huru ni wafungwa waliokuwa wakutumikia kifungo cha chini ya miezi sita au wale ambao walibakisha miezi sita kukamilisha kifungo chao.
Mnamo Aprili mwenyekiti wa NCAJ, Jaji Mkuu David Maraga alitangaza kuwa Mahakama Kuu ilianza kupokea faili za wafungwa wa makosa madogo kuzikagua kabla ya kuwaachilia huru.
Kufuatia shughuli hiyo, wafungwa 4,800 waliachiliwa huru wakati huo kama hatua ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Hatua zingine ambazo Idara ya Magereza Nchini Kenya ilichukua kupambana na janga hili, ni kuanzishwa kwa vituo vya kutenga wafungwa wanaoshukiwa kuambukizwa virusi hivyo na kusikizwa kwa kesi za wafungwa kwa njia ya mtandao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |