Mahakama ya Jumuiya ya Afrika mashariki imetupilia mbali kesi dhidi ya mabadiliko ya katiba nchini Uganda yaliyotoa nafasi kwa rais Yoweri Museveni kugombea muhula mwingine madarakani.
Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Monica Mugenyi Jumatano, mahakama hiyo imeamua kwamba "hatua ya kuondoa ukomo wa umri kwa wagombea wa urais nchini Uganda haikukiuka katiba ya Uganda."
Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha, Tanzania, imemwondolea pia makosa aliyekuwa jaji mkuu wa Uganda Bart Katureebe katika kesi hiyo iliyowasilishwa na wakili wa Uganda Male Mabirizi.
Wakili huyo alikuwa amemshutumu Katureebe kwa kufanya kazi yake bila kuzingatia maadili na kuwa na upendeleo.
Katika kesi yake, wakili Mabirizi alidai kwamba mchakato mzima wa kubadilisha kifungu 102(b) cha katiba ya Uganda, kilichokuwa kimeweka ukomo wa miaka 75 kwa wagombea wa urais nchini Uganda, haukufuata sheria.
Kesi hiyo ilifikishwa katika mahakama ya jumuiya ya Afrika mashariki mwezi May, 2019, ikitaka hatua ya kufanyia marekebisho katiba ya Uganda kufutiliwa mbali.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |