Kanuni kadhaa zinastahili kufuatwa katika kuendeleza uhusiano kati ya China na Ufaransa
2019-03-25 15:53:08| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesema China na Ufaransa ni marafiki wasio wa kawaida. Kwani Ufaransa ni nchi ya kwanza ya magharibi iliyoanzisha uhusiano wa kibalozi na Jamhuri ya Watu wa China, na pia ilitangulia katika kuanzisha ushirikiano na China katika mambo mbalimbali, ikiwemo kuanzisha safari za ndege ya moja kwa moja kati yake na China, kujenga kituo cha utamaduni wa kichina, na kuanzisha idara ya lugha ya kichina katika vyuo vikuu.

Ufaransa inadumisha uhuru katika sera ya kidiplomasia. Ilipinga vita dhidi ya Iraq iliyoanzishwa na Marekani, na kufanya kazi ya uongozi pamoja na China katika suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Hii ndiyo sababu ya Ufaransa kuwa na uhusiano maalumu na China kwa kutofautiana na nchi nyingine.

Katika mawasiliano ya watu na ustaarabu, Ufaransa ina miji 102 ambayo imeanzisha urafiki na miji ya China, na karibu wanafunzi elfu 40 wa China wanasoma nchini Ufaransa, huku zaidi ya wafaransa laki moja wakijifunza lugha ya kichina; Katika mambo ya uchumi na biashara, Ufaransa imedumisha ushirikiano mzuri na China katika uzalishaji wa umeme kwa nishati ya nyuklia, na mwaka jana thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia dola bilioni 62.9 za kimarekani.

Huu ni mwaka wa 55 tangu China na Ufaransa zianzishe uhusiano wa kibalozi, na nchi hizo mbili zinapaswa kufuata kanuni muhimu zilizoleta ufanisi, ikiwa ni pamoja na kujiamulia, kufungua mlango ili kupata mafanikio ya pamoja, kusikilizana na kuigana, na kuwajibika, ambazo zilijumuishwa na rais Xi wa China, ili kuimarisha na kuendeleza zaidi uhusiano huo.

Hivi sasa mabadiliko makubwa yanatokea duniani. Nchi za Ulaya zinarekebisha sera zao za kidiplomasia na nchi nyingine, ikiwemo China. Wakati China na Umoja wa Ulaya zinasukuma mbele ushirikiano wa kuwasiliana na kuungana zaidi, baadhi ya watu wa Ufaransa wanafuatilia pendekezo la China la "Ukanda Mmoja, Njia Moja".

Kanuni ya pendekezo hilo lililotolewa na rais Xi ni "kujadili, kujenga na kunufaika kwa pamoja", maana yake muhimu ni usawa, ushirikiano na mafanikio ya pamoja. China na Ufaransa zinaaminiana kisiasa, na Ufaransa inaweza kupiga hatua kubwa zaidi katika kujiunga na pendekezo la "Ukanda Mmoja, Njia Moja".

Mwaka jana, thamani ya mauzo ya rejareja nchini China ilifikia dola trilioni 5.65 za kimarekani, na ni kubwa zaidi duniani. Soko la China limetoa fursa kubwa kwa wenzi wa kibiashara wa China haswa Ufaransa. Licha ya nishati ya nyuklia na ndege za abiria, pombe, nyama ya ng'ombe, vipodozi, nguo, dawa na bidhaa nyinginezo za Ufaransa zinapendwa sana na wateja wa China. Takwimu zilizotolewa na wizara ya biashara ya China zinaonesha kuwa, katika miezi miwili iliyopita mwaka huu, maagizo ya bidhaa ya China kutoka Ufaransa yaliongezeka kwa asilimia 42.2 ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huu.

Miaka 55 iliyopita, Ufaransa ilifuata sera ya kujiamulia, na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na China. Hivi sasa kutokana na hali ya utatanishi duniani, Ufaransa inatarajiwa kuonesha msimamo huru, ujasiri na busara katika kuendeleza uhusiano kati yake na China.