China ni nchi inayodumisha utulivu wa biashara duniani
2019-04-12 19:41:47| CRI

Takwimu zilizotolewa leo na Idara Kuu ya Forodha ya China zinaonyesha kuwa thamani ya jumla ya uagizaji na uuzaji bidhaa nje wa China katika robo ya kwanza ya mwaka huu ilifikia yuan trilioni 7.01, sawa na dola za kimarekani trilini 1.04, likiwa ni ongezeko la asilimia 3.7.Wakati mvutano wa biashara duniani unaongezeka, na kasi ya ongezeko la biashara duniani inapungua, matokeo iliyopata China katika biashara na nchi za nje katika kipindi hicho, hayakupatikana kwa urahisi, na kuonesha nguvu ya uhimili ya uchumi wa China, na nguvu kubwa iliyojifichika katika soko la China.

Uuzaji na uagizaji bidhaa nje ya China katika robo ya kwanza ya mwaka huu umeonesha sifa ya "kudumisha utulivu na kuongeza ubora", hali ambayo inajikita katika pande tatu, yaani wenzi wa kibiashara wa China wamekuwa wengi, muundo wa bidhaa zinazouzwa nje na kuagizwa kutoka nje umeboreshwa, na injini ya ukuaji wa biashara ya nje imekuwa na nguvu zaidi.

Siku kumi zilizopita, Shirika la Biashara Duniani WTO lilipunguza makadirio ya kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia kutoka asilimia 3.7 hadi 2.6, kiwango ambacho ni chini zaidi katika miaka hii mitatu, sababu muhimu ni kuongezeka kwa mvutano wa kibiashara na sintofahamu kiuchumi. Katika mazingira hayo, biashara ya nje ya China inaweza kudumisha ukuaji tulivu na kuongeza ubora wake, hii sio kazi rahisi.

Kwa upande mmoja, hii inaonesha kuwa uchumi wa China una nguvu kubwa ya uhimili, sio tu unaweza kuhimili changamoto zinazotokana na mvutano wa kibiashara, bali pia unaweza kugeuza changamoto kuwa fursa. Kwa upande mwingine, tangu mwaka jana rais Xi Jinping wa China alipotangaza kwenye Kongamano la Asia la Bo'ao lililofanyika mkoani Hainan, kuwa China itapunguza masharti ya upatikanaji wa masoko ya China kwa nchi za nje, kuandaa mazingira ya uwekezaji yanayovutia zaidi, kuongeza nguvu ya kulinda hakimiliki ya ubunifu na kupanua uagizaji wa bidhaa kutoka nje, hatua husika zimeanza kutekelezwa na kutoa hamasa kubwa kwa makampuni yanayoshughulikia uuzaji na uagizaji bidhaa nje ya nchi na kusaidia maendeleo ya biashara ya nje.

Mkutano wa pili wa kilele wa ushirikiano wa kimataifa wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja" utafanyika baadaye mwezi huu na Maonyesho ya Pili ya Kimataifa ya Uuzaji na Uagizaji Bidhaa pia yatafanyika mwishoni mwa mwaka huu. Hii itakuwa ni fursa kubwa kwa maendeleo ya biashara duniani, na China itaendelea kulinda utulivu wa biashara duniani.