Dhamira na malengo ya Ukanda Mmoja Njia Moja yatoa msukumo kwa mataifa yanayoendelea kuukumbatia mpango huo
2019-04-26 20:34:29| CRI

Na Eric Biegon - NAIROBI

Mwaka 2017 iliashiria hatua ya kihistoria ya uhusiano wa China na ulimwengu. Aidha, mwaka huo ulikuwa wenye matukio mahsusi hasa kwa uhusiano kati ya China na Afrika. Utaratibu mpya wa dunia uliibuka.

Huu ni mwaka ambao dunia ilishuhudia uzinduzi rasmi wa mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja katika mji mkuu wa Beijing na kuashiria mwamko mpya duniani.

Hatua hii ilimaanisha kuwa mahusiano kati ya China na Afrika na ulimwengu mzima yalibadilika kimsingi na kupanuka na kuwa na uwezo wa kabadilisha hatima zao.

Uzinduzi huu ulikuwa wa kihistoria hasa tunapoangazia msingi uliofanikisha kuratibiwa kwake. Kanuni zinazoiongoza, malengo pana, maeneo ya kipaumbele na mifumo ya ushirikiano wake yaliifanya kuwa tofauti na ya kipekee.

Mpango huu unasisitiza juhudi za pamoja kupitia mashauriano ili kuleta manufaa kwa wote, wito wa uratibu wa sera kwa pamoja, muunganisho wa miundombinu, kufanya biashara bila vikwazo, mwingiliano wa kifedha na ujenzi wa mahusiano ya karibu ya watu kutoka mataifa wanachama.

Haya ni vipengele muhimu ya kuleta mafanikio kwa mataifa yote yanayoshiriki mpango huo. Kwa mujibu wa Rais wa China Xi Jinping, China iliongoza juhudi za kuanzishwa kwa mpango huu ili kusaidia kukabiliana na changamoto za kifedha za kujenga miundombinu muhimu na ukosefu wa utaalamu unaofaa.

Tunapoangalia nguzo muhimu za mfumo huu wa ushirikiano, ni rahisi kuelewa ni kwa nini viongozi wengi kutoka mataifa yanayoendelea wamevutiwa. Kutoka siku ya uzinduzi wake wengi walitia saini kujiunga kama wanachama wa mpango huu, huku idadi kubwa ikitoa maombi ya kujiunga.

Mkutano wa mwaka huu wa BRI jijini Beijing imeudhuriwa na viongozi wa mataifa mengi, huu ukiwa ni ushuhuda tosha ya hali ya kukubaliwa kwa mpango huo.

"Kama mdhamini, China iko tayari kuelekeza nia njema kwa washirika wake, kuheshimu ahadi zake na kutimiza majukumu yake." Rais Xi alitangaza 2017.

Tangu wakati huo, bara la Afrika limeshuhudia maendeleo ya miradi mbalimbali ya miundombinu kupitia msaada wa fedha kutoka China. Madaraja, viwanja vya ndege, barabara na miundombinu mengine yamesaidia kubadilisha sehemu kubwa ya Afrika, na kuinua mataifa kufikia awamu mpya ya maendeleo.

Reli ya kisasa ya Standard Gauge nchini Kenya kutoka Nairobi hadi Mombasa ulifadhiliwa na kujengwa na China. Ni mradi uliotekelezwa chini ya mpango wa ukanda mmoja njia moja. Reli hii ilifunguliwa kwa umma mwezi Mei 2017 na baada ya mwaka moja na nusu wa utekelezaji wake, SGR imebeba abiria milioni 2.2. Wakati wa kusafiri pia umepunguzwa na usafirishaji wa bidhaa imefanyika rahisi zaidi. Mradi huu wa reli sasa unaelekezwa Naivasha kabla ya kupanuliwa hadi kwenye mpaka wa Kenya na Uganda.

Nchini Ethiopia, Hawassa Industrial Park ilizinduliwa siku za hivi karibuni. Ni hifadhi kubwa ya viwanda katika Afrika. Sehemu hii ya viwanda inashighulika hasa na bidhaa za nguo na mavazi. Serikali ya Ethiopia inakadiria kwamba watu 60,000 wataajiriwa katika sehemu hiyo ya viwanda.

Tayari, makampuni 18 yanayoshughulika na uzalishaji wa nguo kutoka Marekani, China, India, Sri Lanka yanaendesha shughuli zao ndani ya sehemu hii.

Daraja la Maputo Bay nchini Msumbiji pia ni mradi chini ya mpango wa BRI. Daraja hilo lililojengwa na kampuni ya China ya China Road and Bridge Corporation lilifunguliwa mwaka jana. Inatarajiwa kuwa mradi huo utarahisisha usafiri na muunganisho kati ya Msumbiji na sehemu nyingine za bara la Afrika.

Jumba la Iconic Tower nchini Misri ni nyingine. Misingi yake yanajengwa kwa sasa. Ni moja ya miradi kadhaa mikubwa yaliyozinduliwa na serikali ya Misri katika jitihada za kuchochea uchumi wa taifa hilo lenye wakazi wengi kati ya mataifa ya Kiarabu. Inatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu na nusu.

Hizi ni baadhi ya mifano ya miradi yaliyotekelezwa barani Afrika kwa hisani ya mpango wa ukanda mmoja njia moja. Katika miongo michache yaliyopita, nchi nyingi za Afrika hazikusajili uwekezaji mkubwa kutoka mataifa ya nje. Serikali ya China kwa sasa inayahamasisha makampuni ya Kichina kupanua uwekezaji wao katika nchi ambazo miradi ya BRI yanatekelezwa.

Wakati Marekani na Ulaya yanapata shinikizo ya kisiasa kuhusiana na bajeti na kupunguza msaada wao Afrika, China inajitokeza kama mshirika mkuu wa maendeleo barani humo.

Kutokana na dhamira na malengo yake, mpango wa ukanda mmoja njia moja utasukuma ushirikiano huu kufikia enzi mpya ya maendeleo na matokeo yake ikiwa ni mafanikio kwa kila mmoja.