Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jumatano ilitangaza kupanga kuinua kiwango cha ushuru wa forodha dhidi ya bidhaa za China zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 200 hadi asilimia 25 kutoka asilimia 10 ya awali, hatua ambayo itatekelezwa kuanzia Mei 10. Kuhusu uamuzi huo wa Marekani, China imetoa taarifa ikisema kuongeza mgogoro wa kibiashara kati ya pande hizo mbili hakuendani na maslahi ya watu wa nchi hizo mbili na dunia nzima, China imesikitishwa na uamuzi huo, na kama Marekani ikitekeleza hatua hiyo, China italazimika kuchukua hatua za lazima za kujibu.
Taarifa hizo mbili za Marekani na China zimekuja wakati nchi hizo mbili zinafanya duru ya 11 ya mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu masuala ya uchumi na biashara. Kwa upande wa Marekani, madhumuni yake ya kuongeza shinikizo kwa China yameonekana wazi, na kwa upande wa China, jibu limetolewa kwa haraka na kwa msimamo imara, yaani kama Marekani ikitaka kufanya mazungumzo, mlango uko wazi; kama ikitaka vita vya kibiashara, China pia iko tayari kukabiliana nayo hadi mwisho.
Kutokana na hayo yote watu wanaweza kuona kuwa, pande hizo mbili zinafanya mazungumzo huku zikikabiliana, na huenda hii itakuwa kawaida katika mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani.
Kutatua mgogoro kwa njia ya mazungumzo, ni msimamo ulio wazi wa China. Mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani yameshafanyika kwa duru ya kumi sasa, ambapo pande hizo mbili zimepata maendeleo makubwa kwenye masuala mengi, yakiwemo manunuzi na taratibu za utekelezaji, ambayo hayakupatikana kirahisi, kwa hivyo yanatakiwa kuthaminiwa. Wakati huohuo, bado kuna masuala kadhaa ambayo yanapaswa kujadiliwa zaidi. Kwa hiyo, wakati duru ya kumi ya mazungumzo hayo ilipomalizika, pande hizo mbili zilikubaliana kufanya duru ya 11 ya mazungumzo wiki hii mjini Washington. Ingawa hatua ya Marekani imezusha sintofahamu kwa duru hiyo mpya ya mazungumzo, China bado imeamua kushiriki kwenye mazungumzo hayo kama ilivyopangwa, hali inayoonesha kuwa China inafuata kanuni za mazungumzo, na pia inaheshimu matokeo yaliyopatikana katika miezi 16 iliyopita.
China inaelewa kwa kina kuhusu mgogoro wa kibiashara kati yake na Marekani, kwa hivyo haitaacha kirahisi mbinu zake za utatuzi wa matatizo kutokana na jambo moja au mawili. Uzoefu wa nyuma umedhihirisha kuwa kukabiliana na kuongeza shinikizo kwa upande mwingine hakusaidii kuondoa mgogoro huo, na hatimaye pande mbili zinatakiwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Muhimu zaidi ni kwamba China ni nchi kubwa inayowajibika. Rais Xi Jinping wa China amesisitiza mara kwa mara kuwa mahusiano kati ya nchi kubwa yanahusiana na utulivu wa kimkakati wa dunia nzima, China na Marekani zina maslahi mengi ya pamoja na pia zinabeba majukumu muhimu ya pamoja katika kulinda amani na utulivu wa dunia, na kuhimiza maendeleo ya ustawi wa dunia. Katika zaidi ya mwaka mmoja uliopita, mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani si kama tu umeharibu maslahi ya pande hizo mbili, bali pia umekwamisha ukuaji wa uchumi wa dunia nzima. Ripoti mpya ya Makadirio ya Uchumi wa Dunia iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF imeshusha ongezeko la uchumi wa dunia kwa mwaka huu na mwaka kesho kwa asilimia 0.2 na asilimia 0.1, hadi kufikia asilimia 3.5 na asilimia 3.6 mtawalia.
Duru ya 11 ya mazungumzo ya ngazi ya juu ya uchumi na biashara kati ya China na Marekani itafanyika mjini Washington. China itaendelea kufanya juhudi kwa udhati kurejesha mazungumzo hayo kwenye njia sahihi. Lakini mazungumzo ni ya pande mbili, mafanikio yake yanaihitaji Marekani iende sambamba na China, ili kupunguza tofauti na kupanua ushirikiano.
Bila kujali matokeo ya mazungumzo hayo yatakuwa namna gani, China iko tayari kukabiliana na hali yoyote inayowezekana kutokea, na kuendelea kufuata njia yake ya kuhimiza mageuzi na kufungua mlango zaidi, ili kutimiza maendeleo ya hali ya juu, na kutoa fursa nyingi zaidi ya maendeleo na ushirikiano kwa dunia nzima.