Mitaji ya kimataifa ina imani na soko kubwa la China
2019-05-21 19:46:56| CRI

Takwimu zinaonesha kuwa kutoka mwezi wa Januari hadi Aprili mwaka huu, China imetumia mitaji ya kigeni ya dola bilioni 44.2 za kimarekani, ambayo inaongezeka kwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na mwaka jana. Uwekezaji kutoka vyanzo vikuu vya Korea Kusini, Marekani na Ujerumani umeongezeka kwa asilimia 114.1, 24.3 na 101.1 mtawalia. Vituo vikuu vya kikanda na vituo vya utafiti vya makampuni 27 ya kimataifa vimeanzishwa jijini Shanghai, ambako mitaji ya kigeni iliyotumiwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 20.3 ikilinganishwa na mwaka jana. Katika mkoa wa Hainan ambayo ni eneo maalumu la kiuchumi lenye eneo kubwa zaidi nchini China, mitaji ya kigeni iliyotumiwa imeongezeka mara 20 hivi kwenye miezi minne ya mwanzo ya mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.

Katika hali ambayo mzunguko wa mitaji duniani unapungua, uvutiaji wa uwekezaji wa China umeonesha mwelekeo mzuri na imani ya mitaji ya kimataifa kwa mustakabali wa maendeleo ya China.

Kwanza, imani ya mitaji ya kimataifa inatokana na soko kubwa la China. idadi ya watu karibu bilioni 1.4 na kundi la watu wenye pato la wastani ambalo ni kubwa zaidi na linalokua haraka zaidi duniani, vimeunda soko kubwa la China lenye uwezo mkubwa. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, matumizi yamechangia asilimia 65.1 ya ongezeko la uchumi wa China, ambayo yanaendelea kuwa injini kuu ya kuhimiza ukuaji wa uchumi wa China.

Pili, imani ya mitaji ya kimataifa inatokana na uhai wa soko la China. Katika miezi minne ya mwanzo ya mwaka huu, shughuli za utengenezaji wa teknolojia mpya na ya hali ya juu na huduma za teknolojia ya hali ya juu zimekuwa nguvu mpya ya kuhimiza ukuaji wa uchumi wa China. Takwimu kutoka wizara ya biashara ya China zinaonesha kuwa shughuli za utengenezaji wa teknolojia mpya na za hali ya juu zimetumia mitaji ya kigeni ya dola bilioni 4.83 za kimarekani ambayo inaongezeka kwa asilimia 12.3 ikilinganishwa na mwaka jana. Huduma za teknolojia ya hali ya juu zimetumia mitaji ya kigeni ya dola bilioni 7.6 za kimarekani ikiongezeka kwa asilimia 73.4 ikilinganishwa na mwaka jana.

Tatu, imani hiyo pia inatokana na utulivu wa soko la China. Wakati hali zisizo na uhakika katika mustakabali wa uchumi wa dunia zikizidi kuongezeka, mitaji ya kigeni inatilia maanani katika utulivu na makadirio ya soko la matumizi. Serikali ya China inatumia vifaa mwafaka vya sera kukabiliana na masuala ya maendeleo ya uchumi ya hivi sasa na ya siku za baadaye, kuzidisha kwa pande zote mageuzi na ufunguaji mlango na kujenga mazingira ya kibiashara kuwa ya kimataifa na yenye urahisi yanayofuata sheria, ili kuongeza imani ya mitaji ya kimataifa.

Mitaji ya kimataifa inatumia hatua halisi kuthibitisha ukubwa, uhai, utulivu na mvuto wa soko la China. Rais Xi Jinping wa China katika mkutano wa pili wa kilele wa baraza la ushirikiano wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja" alisema, China itapanua maeneo yanayoruhusu mitaji ya kigeni kuingia, kuongeza ushirikiano wa kimataifa kuhusu kulinda hakimiliki ya ujuzi, kuzidisha kwa kiasi kikubwa uagizaji wa bidhaa na huduma, kutekeleza kwa ufanisi zaidi uratibu wa sera za uchumi wa kimataifa, na kuzingatia zaidi utekelezaji wa sera za kufungua mlango. Nia thabiti na hatua za China haziwezi kuondolewa kwa kelele yoyote, na matarajio kuhusu soko kubwa la China hayatapunguzwa na mtu yeyote.