China yatoa tahadhari kwa wanafunzi wanaotaka kusoma nchini Marekani
2019-06-03 20:20:29| CRI

Wizara ya elimu ya China leo imetoa tahadhari ya kwanza ya mwaka 2019 ikisema, kutokana na kuzuiwa kwa visa za baadhi ya wachina wanaoenda kusoma Marekani, muda wa ukaguzi wa visa kuongezeka, muda wa visa kufupishwa na kiwango cha kukataliwa maombi ya visa kuongezeka, wanafunzi wa China wanaotaka kwenda kusoma nchini Marekani au kumaliza masomo yao nchini humo wanakabiliwa na athari kubwa. Wizara hiyo inawakumbusha wanafunzi na wasomi wengi kuimarisha tathmini ya hatari kabla ya kwenda kusoma nchini Marekani, kuongeza wazo la kujikinga na hatari na kujiandaa vizuri.

Hii ni tahadhari ya 63 kwa wanaosoma nchi za nje iliyotolewa na wizara ya elimu ya China tangu ianzishe mfumo wa tahadhari mwaka 2003, ambayo kiini chake ni visa. Kuanzia mwaka jana, Marekani imeanza kutekeleza hatua ya vizuizi vya visa dhidi ya baadhi ya watu wa China wanaoenda nchini Marekani kwa kisingizio cha ujasusi. Kamati ya kijeshi ya baraza la chini la Marekani imetoa mswada wa idhini ya ulinzi wa taifa ukitaka kuimarisha ukaguzi wa maombi ya visa yanayotolewa na wanafunzi na watafiti wa China.

Kutokana na athari hizo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na kamati ya udhamini wa masomo ya China, kati ya watu 10,313 waliopangwa kutumwa na serikali ya China kusoma nchini Marekani mwaka 2018, watu 331 walishindwa kwenda kusoma nchini Marekani kutokana na matatizo ya visa. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, watu 182 kati ya 1,353 waliopangwa kutumwa na serikali ya China kwenda kusoma nchini Marekani wameshindwa kusoma nchini humo kutokana na suala la visa.

Katika hali ambayo mikwaruzano ya kibiashara kati ya China na Marekani inaendelea kupamba moto, Marekani inayachukulia mawasiliano ya elimu kati yake na China kama shughuli za kisiasa. Hatua hiyo sio tu inaharibu heshima ya wanafunzi wa China na maslahi yao halali, bali pia yanaathiri vibaya ushirikiano wa elimu kati ya nchi hizo mbili. Tahadhari hiyo iliyotolewa na China kwa watu wa China wanaotaka kwenda kusoma nchini Marekani au wanaosoma nchini humo inalenga kulinda maslahi yao, ambayo pia ni hatua ya lazima ya kukabiliana na hali mbaya ya mazingira ya elimu ya Marekani.

Vitendo hivyo vya wanasiasa wa Marekani haviwezi kuwadanganya wadau wa elimu ya Marekani. Hivi karibuni kamati mbili za elimu ya juu za Marekani zimetoa taarifa ikisema, wanafunzi wa China wanaosoma nchini Marekani ni muhimu sana kwa utafiti wa sayansi. Wakuu wa vyuo vikuu vingi vya Marekani vinavyojulikana duniani ikiwemo Harvard, Yale na Stanford wote wametoa taarifa ikiwakaribisha na kuwaunga mkono wanafunzi na wasomi wa China. Ni wazi kwamba, baadhi ya wanasiasa wa Marekani wameutumia ushirikiano wa elimu kama silaha ya kisiasa, ambayo imeathiri maslahi ya vyuo vikuu vya Marekani na nguvu yao ya ushindani wa kimataifa.