Kauli ya Marekani kwamba imepata hasara katika biashara kati yake na China haina msingi
2019-06-06 19:58:33| CRI

Wizara ya biashara ya China leo imetangaza ripoti ya utafiti kuhusu faida inayopata Marekani katika ushirikiano wa kibiashara kati yake na China, ikionesha hali halisi na chanzo cha urari mbaya wa biashara kwa Marekani, lakini pia inaonesha kuwa Marekani imepata faida kubwa kutokana na ushirikiano wa biashara kati yake na China, na ingawa China ina urali mzuri wa biashara, lakini pande zote mbili zinanufaika, na kwamba kauli kuwa Marekani ni upande unaopata hasara haina msingi.

Hii ni ripoti inayotolewa na China kuhusu utafiti kuhusu pengo la biashara kati ya Marekani na China baada ya kutolewa kwa waraka kuhusu msimamo wa China juu ya mazungumzo ya biashara kati ya China na Marekeani tarehe 2 mwezi huu, ambao umefafanua zaidi msimamo na mawazo ya China kuhusu waraka iliotoa, na kusaidia jumuiya ya kimataifa kutambua vizuri zaidi ukweli wa mambo kuhusu pengo la biashara kati ya Marekani na China.

Kisingizio cha Marekani cha kuongeza ushuru ni kwamba kuna urari mbaya wa dola za kimarekani bilioni 500 kwenye biashara kati yake na China, na kwamba Marekani inapata hasara wakati China inafaidika. Ripoti hiyo iliyotolewa na Wizara ya biashara ya China imethibitisha kuwa takwimu za biashara zinazotolewa na Marekani si sahihi, na kutoa mahesabu kwamba kiasi cha urari wa biashara wa Marekani kwa China ulikuwa dola za kimarekani bilioni 153.6 katika mwaka 2018, ambao ni asilimia 37 ya takwimu zilizotolewa na Marekani.

Kutokana na ukweli wa mambo, biashara kati ya China na Marekani inaamuliwa na soko, na ni matokeo ya chaguo la hiari la makampuni na wateja wa nchi hizo mbili. Marekani kuihusisha hali hii na China peke yake, na kujidai kuwa inapata hasara, ni kinyume na kanuni ya kimsingi ya uchumi na biashara ya kimataifa, na kanuni za lazima katika ushirikiano kati ya makundi ya uchumi. Madhumuni yake ni kuilazimisha China isalimu amri bila msingi, na kuipa faida yote Marekani, kitendo ambacho ni umwamba.

Hivi karibuni mbali na kuongeza ushuru kwa bidhaa za China, Marekani imefanya vita ya biashara na Mexico na India, huku ikiongeza shinikizo kwa Umoja wa Ulaya na Japan, lengo lake ni kuwafanya wenzi hao wa biashara kutoa kipaumbele kwa maslahi ya Marekani kwa kudhuru maslahi yao. Nyaraka mbalimbali zilizotolewa na serikali ya China zitaisaidia jumuiya ya kimataifa kutambua vizuri jinsi Marekani inavyotumia umwamba, ambazo zina umuhimu katika kuzifanya nchi mbalimbali zilinde vizuri zaidi maslahi na heshima za nchi, na kanuni za biashara ya kimataifa ya pande nyingi.

China siku zote inayawekea mazungumzo kuwa chaguo la kwanza la kutatua mgogoro wa kibiashara, lakini lazima yafanyike kwenye msingi wa kuheshimiana, usawa na kunufaishana.