China yaingia katika zama ya matumizi ya kibiashara ya teknolojia ya 5G kwa njia ya kufungua mlango na kunufaishana
2019-06-06 17:35:27| CRI

Wizara ya viwanda na TEHAMA ya China leo imetangaza kutoa leseni kuhusu matumizi ya kibiashara ya teknolojia ya 5G kwa makampuni manne ya mawasiliano ya simu yakiwemo China Mobile, China Telecom, China Unicom na Mtandao wa Matangazo wa China (China Broadcast Network). Hatua hii imeonesha kuwa China imefungua rasmi zama ya matumizi ya kibiashara ya teknolojia ya 5G, na kuwa soko kubwa zaidi la teknolojia hiyo duniani litakalotoa fursa nyingi mpya, kuhimiza mageuzi mapya ya viwanda, kutoa huduma mpya kwa maisha ya wananchi, na kuongoza ukuaji wa uchumi duniani.

Utoaji wa leseni ya matumizi ya kibiashara ya teknolojia ya 5G ni habari iliyosubiriwa kwa hamu na masoko ya nchi mbalimbali duniani. Hivi sasa nchi zilizoendelea duniani zimeingia katika kipindi cha kuandaa mipango kwa ajili ya teknolojia hiyo. Wiki iliyopita kampuni ya mawasiliano ya simu nchini Uingereza EE ilianzisha utoaji wa huduma ya 5G katika miji sita nchini humo, na Shirika la Utangazaji la nchi hiyo BBC lilitangaza moja kwa moja hali hiyo kwa kutumia teknolojia na vifaa ya 5G zilizotolewa na Kampuni ya Huawei ya China.

Hivi sasa teknolojia na bidhaa za 5G za China zinaendelea kukamilika, sehemu muhimu kwenye mnyonyoro wa viwanda hivyo imefikia kiwango cha matumizi ya kibiashara. Majaribio ya teknolojia ya 5G ya makampuni za mawasiliano ya simu zikiwemo China Telecom, China Mobile na China Unicom yamekuwa yakiendelea katika sehemu mbalimbali kote nchini China, na mipango kuhusu kufungua vituo vya 5G imetangazwa katika miji mingi ikiwemo Shanghai na Guangzhou.

Utafiti na uendelezaji wa 5G hauwezi kufanywa kwa nchi moja au kampuni moja. Hiki ni kipindi muhimu kwa kufanya utungaji wa vigezo, utafiti na uendelezaji wa teknolojia na utengenezaji wa bidhaa za teknolojia hiyo, ambayo vigezo vyake vinapaswa kuwekwa kwa kuhusisha viwanda vya sekta hiyo duniani na kuwa vigezo vya pamoja vya kimataifa, na makampuni ya China yameongoza duniani katika teknolojia muhimu.

Teknolojia ya 5G ya China itatumiwa kibiashara, na makampuni mengi ya kigeni ikiwemo Nokia yameshiriki kwenye ujenzi wa mtandao wa teknolojia hiyo, hivyo kuonesha mnyonyoro wa utoaji wa huduma ya teknolojia duniani hautaweza kuzuiliwa kwa kuingiliwa kwa nguvu kutoka nje. Serikali ya Marekani imetangaza marufuku ya matumizi ya vifaa vya Huawei kwa makampuni nchini humo, na kuzishinikizia nchi au sehemu nyingine kusimamisha ushirikiano na kampuni hiyo. Shirika la habari la Marekani CNN limesema hatua hizo zitayaletea makampuni ya nchi hiyo hasara ya dola za kimarekani bilioni 11. Kampuni ya mawasiliano ya simu ya mkononi ya Uingereza EE, na Kampuni ya mawasiliano ya simu ya nchi hiyo Vodafone pia zimetangaza kuwa, zitaendelea kutumia vifaa vya wireless vya teknolojia ya 5G kutoka Kampuni ya Huawei.

Wachambuzi wanaona kuwa, China inatarajiwa kuandaa soko la 5G lenye idadi ya watumiaji milioni 430 kati ya mwaka 2020 na 2025, na kuleta ukuaji wa uchumi wenye thamani ya dola za kimarekani trilioni 1.54.

Matumizi ya kibiashara ya teknolojia ya 5G yataleta fursa mpya za viwanda na nafasi mpya za ajira nchini China, na pia kuwanufaisha zaidi watu wa nchi mbalimbali. China inapenda kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya teknolojia hiyo kutokana na sifa zake za teknolojia na viwanda. Vilevile inayakaribisha makampuni na mitaji kutoka nchi mbalimbali kushiriki katika ujenzi wa mtandao wa 5G, pamoja na matumizi na uenezi wake. Yeyote anayejaribu kutawala na kuendeleza teknolojia hiyo kwa upande wake kipekee, kutaweza tu kudhuru kiwango chake cha teknolojia na kushindwa kwenye ushindani.