China na Marekani zinaweza kutatua mgogoro wao wa kibiashara kama zikifanya mazungumzo kwa usawa
2019-06-20 19:07:40| CRI

Marais wa China na Marekani Jumanne walizungumza kwa njia ya simu, wakisema watakutana tena kwenye mkutano wa wakuu wa kundi la G20 mjini Osaka, Japan. Pia wamekubaliana kudumisha mawasiliano kati ya timu za biashara za pande hizo mbili. Habari hii ilituliza kwa kiasi wasiwasi wa watu na kulipa nguvu soko la hisa duniani.

Kutokana na ongezeko la migogoro ya kibiashara na hali tete ya kiuchumi, Shirika la Biashara Duniani WTO hivi karibuni lilishusha makadirio ya ukuaji wa biashara ya kimataifa kutoka asilimia 3.7 hadi asilimia 2.6, huku Benki ya Dunia ikishusha kasi ya ukuaji wa uchumi duniani katika mwaka huu na mwaka kesho hadi kuwa asilimia 2.6 na asilimia 2.7, ambazo ni punguzo la asilimia 0.3 na 0.1 kutoka makadirio yaliyotolewa mwezi Januari. China, ikiwa kundi la kiuchumi linalowajibika, siku zote inaweka kipaumbele majadiliano, kama chaguo la kwanza, kuwasiliana na Marekani na kutarajia kupata ufumbuzi wa mvutano kati yao mapema iwezekanavyo ili kulinda ukuaji wa uchumi wa dunia na maslahi ya watu.

Hata hivyo, China inaona ushirikiano una mstari wa mwisho, na majadiliano yana kanuni. Cha muhimu kwa mazungumzo ya kibiashara kati ya China na Marekani, ni pande hizo mbili kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na marais wa nchi hizo mbili walipokutana mwishoni mwa mwaka jana nchini Argentina, kufanya juhudi kwa pamoja, kufanya mazungumzo kwa usawa na kuheshimu ufuatiliaji wa upande mwingine katika msingi wa kuheshimiana, kusaidiana na kunufaishana.

Baada ya mazungumzo ya simu kati ya marais wa nchi hizo mbili, mjumbe wa biashara wa Marekani Robert Lighthizer alitoa kauli za kushangaza katika mkutano wa baraza la Seneti kuhusu mvutano wa kibiashara kati ya China na Marekani. Alipotoa maelezo mbele ya kamati ya fedha ya Seneti, Lighthizer alisema, mazungumzo hayawezi kutatua mvutano, na alipoulizwa itakuwaje kama mazungumzo hayo yanashinikiza, alisema hadi sasa hakuna njia bora zaidi kama ushuru wa forodha. Alipotoa maelezo kwenye kamati ya uchangiaji fedha ya baraza la wawakilishi, Lighthizer alisisitiza umuhimu wa kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kulinda nguvu ya ushindani ya Marekani katika kutatua mvutano huo.

Kwa upande mmoja, kauli za Lighthizer zimeonyesha nia ya kuanzisha tena mazungumzo ya kibiashara na kuboresha uhusiano kati ya China na Marekani, lakini wakati huohuo, zimetoa ishara ya kutoa shinikizo la ushuru wa forodha. Ni wazi kuwa huu sio mtazamo sahihi wa kutatua tatizo. Hali halisi ya mwaka mmoja uliopita imeonyesha kuwa, katika kutatua mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani, mbinu inayotumiwa na Marekani ya kutoa shinikizo la juu dhidi ya China haikufanya kazi sasa, na baadaye pia haitafanya kazi. Watu wameona tangu Marekani iongeze ushuru wa forodha dhidi ya bidhaa za China zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 200 zinaoingia nchini humo mwezi Mei, China imechukua hatua mfulululizo za kuijibu: kuanzia tarehe mosi, Juni, China imeongeza ushuru wa forodha dhidi ya bidhaa za Marekani zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 60 zinazoingia nchini China, kutoa onyo kuwa Marekani haitakiwi kujaribu kutumia vifaa vinavyotengenezwa kwa madini ya rare earth ya China kuzuia maendeleo ya China, na kuanzisha mfumo wa "makampuni ya kigeni yasiyotegemewa", hatua ambazo zinazidi kupevuka na kuwa za thabiti, China iko tayari kujibu hatua hizo za Marekani.

"Heshima, uaminifu, usawa na kusaidiana" ni kanuni za China kufanya mazungumzo, na Marekani inatakiwa kufahamu ufuatiliaji mkuu wa China, na kufahamu mstari mwekundu na wa mwisho wa China haupaswi kuvukwa.

Bado zinasalia siku 10 kabla ya mkutano kati ya marais wa China na Marekani mjini Osaka, na inatarajiwa kuwa timu za biashara za pande hizo mbili zinaweza kufuata makubaliano yaliyofikiwa na marais hao nchini Argentina, kwenda pamoja, na kufanya mazungumzo juu ya jinsi ya kutatua mvutano wao. Kama Marekani inaendelea kufanya mazungumzo huku ikitumia mbinu ya kuongeza ushuru, itaongeza makali ya mvutano huo.