China kuyawekea vikwazo makampuni ya Marekani yanayoiuzia silaha Taiwan ili kulinda kithabiti maslahi ya taifa
2019-07-14 17:37:23| CRI

Wizara ya mambo ya nje ya China tarehe 12 ilitangaza kuyawekea vikwazo makampuni ya Marekani yanayohusika na kuiuzia silaha Taiwan kutokana na Marekani kutangaza mpango wa kuiuzia Taiwan silaha zenye thamani ya dola bilioni 2.2 za kimarekani hivi karibuni.

Katika taarifa yake hiyo, wizara ya mambo ya nje imesema hatua hii ya China ni ya lazima katika kulinda maslahi yake makuu ya taifa.

Ifahamike kuwa Taiwan ni sehemu isiyotengana na China. Hivyo taarifa inasema kitendo cha Marekani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, kanuni za kawaida za uhusiano wa kimataifa, pamoja na kanuni ya kuwepo kwa China moja na taarifa tatu za pamoja za China na Marekani.

Taarifa imesisitiza kuwa kitendo hicho cha makampuni ya Marekani kuiuzia Taiwan silaha si shughuli ya kibiashara, bali ni kitendo cha kuharibu mamlaka ya nchi na kuingilia mambo ya ndani ya China, na China haitakubali kamwe. China imeweka bayana msimamo wake imara juu ya kulinda maslahi ya taifa na ukamilifu wa ardhi. Hivyo kitendo chochote kitakachoharibu maslahi, umoja, ukamilifu wa ardhi na usalama wa China kitapata hasara kubwa.