Nchi za magharibi zatakiwa kujifunza uzoefu wa mapambano dhidi ya ugaidi wa Xinjiang
2019-07-16 19:47:20| CRI

Hivi karibuni mabalozi wa nchi 37 ikiwemo Russia, Saudi Arabia na Pakistan katika ofisi za umoja wa mataifa mjini Geneva, wametoa barua ya pamoja kwa mwenyekiti wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa na mjumbe mwandamizi wa mambo ya haki za binadamu, ikipongeza maendeleo ya shughuli za haki za binadamu na mafanikio ya mapambano dhidi ya ugaidi na kazi za kuondoa msimamo mkali yaliyopatikana mkoani Xinjiang, China. Hii inamaanisha kuwa jumuiya ya kimataifa ina tathmini ya haki kwa maendeleo ya Xinjiang, na jaribio la baadhi ya nchi za magharibi kuilaumu Xinjiang na kuishinikiza China kwa kisingizio cha suala la "Haki za Binadamu" halitafanikiwa. Nchi hizo zinatakiwa kujifunza uzoefu wa Xinjiang katika mapambano dhidi ya ugaidi na kuutumia katika utatuzi wa masuala yao.

Nchi nyingi kati ya nchi 37 zilizotoa barua ya pamoja ni nchi za kiislamu, na wanadiplomasia wao mwezi Juni mwaka huu walitembelea Xinjiang na kujionea kwa macho yao maendeleo ya kasi ya uchumi wa huko, na jamii yenye utulivu. Tathmini yao kuhusu suala la Xinjiang inaaminika zaidi. Lawama na shutuma zisizo na msingi ambazo zinatolewa na nchi 22 za magharibi haziwezi kuaminika. Nchi hizo zinatumia kisingizio cha haki za binadamu kuingilia siasa za ndani ya China kupitia suala Xinjiang.

Katika muda mrefu uliopita, baadhi ya nguvu za kisiasa za nchi za magharibi na vyombo vya habari vimekuwa vinatunga habari za uwongo kuvichafua vituo vya mafunzo ya kiufundi vinavyoondoa msimamo mkali mkoani Xinjiang kuwa kambi za wafungwa, huku vikishambulia mapambano halali dhidi ya ugaidi ya China na sera za kuondoa msimamo mkali.

Habari hizo za uongo zinapuuza kabisa historia na hali ya hivi sasa ya Xinjiang. Tangu miaka ya tisini ya karne iliyopita, nguvu tatu za uovu mkoa huo zilifanya mashambulizi makali ya kigaidi ambayo yalisababisha vifo na majeruhi ya watu wengi na kuharibu maendeleo ya jamii ya huko. Hivyo, serikali ya China imechukua hatua kulinda utulivu wa jamii ya Xinjiang na kupambana na magaidi.Mbali na hayo, serikali ya China ilizindua vituo vya mafunzo ya kiufundi ili kuwaelimisha watu waliofanya uhalifu mdogo. Vituo hivi vinatoa mafunzo ya lugha, ujuzi wa sheria, ufundi na kuondoa msimamo mkali, ili kung'oa mizizi ya ugaidi na msimamo mkali wa kidini, na kutokomeza shughuli za kigaidi kabla ya kutokea.

Ukweli umethibitisha kuwa uzinduzi wa vituo vya mafunzo ya kiufundi umepata mafanikio. Hadi sasa matukio ya kigaidi hayajatokea katika mkoa wa Xinjiang katika miaka mitatu iliyopita. Mwaka jana pato la mkoa wa Xinjiang liliongezeka kwa asilimia 6.1 ikilinganishwa na la mwaka juzi, na idadi ya watalii ilizidi milioni 150 ambayo iliongezeka kwa asilimia 40. Xinjiang inatumia pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" kunufaika na fursa kubwa zaidi ya maendeleo.

Nchi za magharibi pia zinaathiriwa vibaya na ugaidi, baadhi ya nchi za magharibi zinatakiwa kwenda Xinjiang kuona hali halisi na kujifunza uzoefu wake katika mapambano dhidi ya ugaidi, ili kutatua changamoto zao dhidi ya kigaidi.