FedEx yastahili adhabu kutokana na kukiuka maslahi ya wateja wa China
2019-07-26 18:56:45| CRI

Hivi karibuni idara husika za serikali ya China zimefanya uchunguzi kuhusu kesi ya Kampuni ya Usafirishaji ya Marekani FedEx kutosafirisha vifurushi vya wateja wa China kwa anwani iliyopewa, na kugundua kuwa madai yake kwamba kwa bahati mbaya imekosea kusafirisha vifurushi vya Kampuni ya Huawei kwa Marekani si kweli, na wakati huohuo, FedEx inatuhumiwa kuchelewa kusafirisha zaidi ya vifurushi 100 vya Huawei kwa China.

Uchunguzi huo kwa FedEx umejibu ufuatiliaji wa umma kwa wakati, na kuonesha nia ya China ya kulinda maslahi ya wateja kwa mujibu wa sheria. Aidha, umethibitisha kuwa kampuni yoyote iliyoko nchini China haina haki maalulmu ya kukiuka sheria, na ni lazima FedEx itoe majibu yatakayowaridhisha wateja wa China.

Ikiwa moja ya kampuni kubwa zaidi za usafirishaji za Marekani, FedEx iliingia soko la China miaka 30 iliyopita, hivyo inapaswa kufahamu vizuri sheria ya China na kuwa na moyo wa kufuata makubaliano ya kibiashara. Lakini baada ya serikali ya Marekani kuiweka Huawei kwenye orodha nyeusi mwezi Mei mwaka huu, mara nyingi FedEx, kwa siri, imefanya vibaya dhidi ya vifurushi vya Huawei. Baada ya kugunduliwa, kwanza ilikanusha, kisha ilidai makosa hayo hayakukusudiwa. Sasa uchunguzi unaonesha kuwa FedEx imesema uwongo tena.

Aidha uchunguzi huo pia umegundua kuwa FedEx inatuhumiwa kuacha zaidi ya vifurushi 100 vya Huawei vinavyotakiwa kuingia nchini China kwa makusudi. Hali hii inaleta mashaka kuwa kampuni hiyo inashirikiana na serikali ya Marekani kufanya "utawala wa kuvuka mipaka". Tarehe 24 mwezi Juni, FedEx iliishtaki wizara ya biashara ya Marekani kwa kukiuka katiba ya nchi hiyo kwa kuzilazimisha kampuni za umma za usafirishaji kushirikiana na wizara hiyo, na kudhihirisha uhusiano wa kisiri kati yake na serikali ya Marekani.

Mbali na hayo, China pia imegundua vitendo vingine vya FedEx vinavyokwenda kinyume na sheria za China.

China inakaribisha kampuni za nje kuwekeza nchini humo, sharti ni kwamba, zinafuata sheria za China, kanuni za soko, na makubaliano ya kibiashara. Hivi sasa China imeanzisha mfumo wa "orodha za kampuni zisizoaminika", na itachukua hatua za lazima za kisheria dhidi ya kampuni hizo. Hivyo kampuni za nje zinapaswa kufuata sheria za China kwa makini ili kupata muskatabali mzuri nchini China.