Uchambuzi: Marekani inapaswa kubeba lawama ya kukwama kwa biashara ya mazao ya kilimo kati yake na China
2019-08-06 16:55:05| CRI

Tume ya Ushuru wa Forodha ya Baraza la Serikali la China imetangaza kuwa, kuna uwezekano wa kuongeza ushuru kwa mazao ya kilimo ya Marekani yaliyonunuliwa baada ya tarehe 3, Agosti, na kuzitaka kampuni husika za China zisimamishe kununua bidhaa hizo kutoka Marekani. Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani kutishia kuongeza ushuru wa asilimia 10 dhidi ya bidhaa za China zinazouzwa nchini Marekani zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 3000 kuanzia tarehe mosi, Septemba.

Hii ni hatua ya lazima inayochukuliwa na China ili kujibu kitendo cha Marekani cha kutumia tena fimbo ya ushuru, hivyo ni sahihi na haki. Ukweli ni kuwa, China na Marekani zinasaidiana katika sekta ya kilimo, na biashara ya mazao ya kilimo inalingana na maslahi ya nchi zote mbili. Baada ya marais wa China na Marekani kukutana mjini Osaka, Japan, China ilinunua mazao mengi ya kilimo ya Marekani kwa mujibu wa mahitaji ya ndani na kanuni ya soko. Kuanzia mkutano wa Osaka hadi mwishoni mwa mwezi Julai, soya tani milioni 2.27 kutoka Marekani zilipakiwa katika meli na kusafirishwa kwa China, na kuanzia tarehe 18, Julai, kampuni husika za China zilianza kuuliza bei kuhusu mazao ya kilimo ya Marekani. Hadi usiku wa tarehe 2, Agosti, bidhaa kadhaa ikiwemo soya tani laki 1.3, mtama tani laki 1.2, mabunda ya nyasi kavu elfu 75, ngano tani elfu 60, nyama ya nguruwe na bidhaa zake tani elfu 40 na bidhaa nyingine ziliagizwa, na kampuni za China zilitoa ombi kwa Tume ya Ushuru wa Forodha ya Baraza la Serikali la China kuacha kutoza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa hizo.

China imechukua hatua halisi kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa Osaka, na hii imeonyesha nia nzuri ya China ya kushirikiana na Marekani, ambayo hata hivyo haitekelezi ahadi zake na kutumia fimbo ya ushuru dhidi ya China, kitendo ambacho kimeharibu mazingira ya kimsingi ya China na Marekani kuendelea kufanya biashara ya mazao ya kilimo. Ndiyo maana, China haina budi kuchukua hatua dhidi ya manunuzi ya mazao ya kilimo ya Marekani, ili kulinda uadilifu wa taifa na maslahi yake yenyewe. Wakati huohuo, inataka kuweka wazi kuwa China haiogopi shinikizo lolote la juu, na itajibu kitendo kama hicho kama ilivyoahidi. Marekani inapaswa kubeba lawama juu ya kukwama huku kwa biashara ambayo ingezinufaisha pande zote mbili, na pia itawajibika kwa matokeo yoyote mabaya.

Inasikitisha kuona kuwa, sekta ya kilimo ya Marekani na wakulima watakuwa wahanga wakubwa kutokana na baadhi ya watu wa Marekani kushindwa kufuata ahadi. Gazeti la The Los Angeles Times limesema vita ya kibiashara inaleta hasara kubwa uchumi wa kilimo wa Marekani. Aliyekuwa mkurugenzi wa kamati ya uchumi ya Ikulu ya Marekani Gary Cohn amesema kuongeza ushuru hakutaathiri kihalisi uchumi wa China, lakini sekta ya kilimo ya Marekani inaathiriwa vibaya zaidi.

Watu wanafahamu kuwa China ina watu bilioni 1.4, na ni soko kubwa na lenye nguvu kubwa ya manunuzi. Kama mazao ya kilimo ya Marekani yana bei nzuri na ni bora, yanaweza kupata faida kubwa katika soko la China.

Kama baadhi ya wamarekani kweli wanazingatia maslahi ya wakulima wa Marekani, wanapaswa kutambua ipasavyo hali ya sasa, kusikiliza madai ya wakulima, kuhesabu faida na hasara, na kushirikiana na China kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Osaka ili kutoa mazingira yanayohitajika kwa ushirikiano wa kilimo kati ya nchi hizo mbili.