China kulinda kithabiti maslahi yake
2019-08-15 20:16:01| CRI

Serikali ya China imesema itachukua hatua ya kulipiza kisasi baada ya ofisi ya mjumbe wa biashara wa Marekani kutangaza kuongeza asilimia 10 ya ushuru dhidi ya bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 300 za kimarekani kutoka China.

Hii ni hatua ya lazima inayochukuliwa na China. Hatua ya Marekani imekiuka makubaliano yaliyofikiwa na marais wa nchi hizo mbili huko Argentina na Osaka. Kwa mujibu wa Makubaliano hayo mawili pande mbili za China na Marekani zinatakiwa kutatua masuala kupitia mazungumzo. Lakini Marekani inainua tena fimbo ya ushuru na kwenda kinyume cha njia sahihi ya kutatua masuala hayo. Ingawa upande wa Marekani umesema utaahirisha kuongeza ushuru dhidi ya baadhi ya bidhaa za China, lakini kama haitaondoa ushuru huo, maslahi ya Chinayataharibiwa. Ni halali kwa China kuchukua hatua ya kulipiza kisasi.

Hakuna mshindi katika vita vya kibiashara, kupandisha ngazi ya mikwaruzano ya kibiashara kunaleta madhara kwa pande zote mbili na dunia nzima. China inapenda kufuata njia ya ushirikiano kutatua suala hili. Lakini ushirikiano una kanuni za msingi, mazungumzo yana mstari wa mwisho, China haitarudi nyuma katika masuala ya msingi. China haipendi kufanya vita vya kibiashara, lakini haiogopi kufanya vita hivyo, itafanya vita hivyo katika wakati wa lazima na haitabadilisha msimamo huo. China inafungua mlango kwa mazungumzo, pia iko tayari kufanya vita vya kibiashara hadi mwisho.