Uchambuzi: jaribio la Marekani kulihusisha suala la Hong Kong kwenye mazungumzo ya kibiashara kati yake na China litashindikana
2019-08-31 17:33:16| CRI

Kwa mara nyingine tena, baadhi ya wamarekani Ijumaa walidai kuwa mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na China yanahusiana na suala la Hong Kong, lakini mwezi mmoja uliopita, ni watu hawa walisema wazi kuwa "Hong Kong ni sehemu ya China, na wanaweza kushughulikia wenyewe na hawahitaji ushauri."

Kitu wanachojali watu hao sio utulivu wa Hong Kong, bali wanatumia suala la Hong Kong kama karata yao na kujaribu kuitumia kuipa China shinikizo kwenye mazungumzo ya kibiashara ili kujipatia faida zaidi.

Suala la Hong Kong ni mambo ya ndani ya China, na serikali ya China inatumia mamlaka yake mkoani humo kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Kimsingi ya Hong Kong, nguvu yoyote au mtu yeyote kutoka nje hawana mamlaka ya kuingilia.

China siku zote inadai kuwa ajenda pekee inayojadiliwa katika mazungumzo ya kibiashara ni biashara, na kutaja ajenda nyingine kunaweza kuongeza ugumu katika kutatua matatizo yaliyopo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Biashara ya Marekani, uchumi wa Marekani katika robo ya pili ya mwaka huu uliongezeka kwa asilimia mbili tu, kiasi ambacho ni kidogo kuliko asilimia 3.1 ya robo ya kwanza. Vilevile takwimu zilizotolewa na kamati ya taifa ya biashara kati ya Marekani na China zimesema kutokana na kutoza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa za China zinazoingia Marekani, kwa wastani kila mwaka kila familia nchini Marekani inaongeza matumizi ya dola za kimarekani elfu moja.

Katika mazingira hayo, baadhi ya wamarekani wameeleza kufanya mazungumzo ya kibiashara na China uso kwa uso. Lakini, China inaona kuwa kufuta nyongeza ya ushuru kwa bidhaa za China zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 550 na kuepusha vita vya kibiashara kuzidi kuwa vikubwa zinatakiwa kuwa kazi za vipaumbele.