China yabeba wajibu wa usalama wa nyukilia duniani
2019-09-03 19:25:37| CRI

Kwa mara ya kwanza, serikali ya China leo imetoa waraka kuhusu shughuli za kuhakikisha usalama wa nyukilia, ambapo imejulisha maendeleo ya shughuli hizo, kanuni na sera za kimsingi, mawazo ya usimamizi na uzoefu wake katika kudumisha usalama wa nyukilia, na kufafanua nia na hatua yake ya kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja katika usalama wa nyukilia.

Nishati ya nyukilia ni moja ya matokeo makuu ya sayansi katika karne iliyopita. Hata hivyo matumizi ya silaha za nyukilia yalileta maumivu makubwa kwa binadamu wote, huku ajali za nyukilia za Chernobyl na kisiwa cha Fukushima zikisababisha wasiwasi mkubwa kwa watu. Namna ya kudumisha uwiano wa matumizi ya nishati ya nyukilia na usalama wake, ni suala linalofuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa.

Waraka huo umesisitiza kuwa usalama wa nyukilia hauna mipaka, na kutumia nishati ya nyukilia ni matumaini ya pamoja ya binadamu wote. Ikiwa nchi kubwa, China itaendelea kubeba majukumu ya kukabiliana na matishio na changamto ya usalama wa nyukilia, na kutoa mchango ipaswavyo katika kuinua kiwango cha usalama wa nyukilia, na kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja katika usalama huo.