China yajitahidi kuhimiza mazungumzo ya kibiashara na Marekani kupiga hatua
2019-09-05 18:46:16| CRI

Msemaji wa wizara ya biashara ya China Bw. Gao Feng, amesema China na Marekani zinajadili mpango wa mazungumzo ya duru ya 13 ya kibiashara ambayo yanatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Oktoba mjini Washington. Amesema China itajitahidi kuhimiza mazungumzo hayo kupiga hatua. Hata hivyo amesema China haifikirii kuondoa mashtaka dhidi ya Marekani ambayo imeongeza ushuru wa bidhaa za China zenye thamani ya dola bilioni 300 za kimarekani kwenye Shirika la Biashara Duniani WTO.

Radio China Kimataifa imetoa tahariri ya "mazungumzo ni njia pekee ya kutatua masuala", ikisema pande hizo mbili zimekubali kufanya mazungumzo tena, hali ambayo inalingana na matumaini ya watu wa nchi hizo na wa dunia nzima.

Tahariri hiyo inasema historia na hali halisi vimethibitisha kuwa vita ya kibiashara haitanufaisha upande wowote. Badala ya kutatua masuala, kuongeza ushuru kutaumiza pande zote. Mvutano wa kibiashara kati ya China na Marekani unapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Tahariri hiyo inasisitiza kuwa, pande hizo zinatakiwa kuonesha udhati na kuchukua hatua halisi katika kusukuma mbele mazungumzo, na zikifanya juhudi kwa pamoja zinaweza kutatua masuala.