China na Marekani zaweka mazingira ya kusaidia mazungumzo kwa moyo wa dhati na vitendo halisi
2019-09-12 17:22:38| CRI

Rais Donald Trump wa Marekani jana jioni alitoa taarifa akitangaza kuwa, Marekani itaahirisha hatua ya kuongeza ushuru dhidi ya bidhaa za China zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 25 kutoka Oktoba 1, hadi Oktoba 15. Siku moja kabla ya hapo, China ilitangaza orodha ya awamu ya kwanza ya bidhaa za Marekani ambazo zitasamehewa kuongezwa ushuru, ili kupunguza athari mbaya zinazotokana na mgogoro wa uchumi na biashara kwa makampuni ya kigeni nchini China.

Kwa mujibu wa mazungumzo kati ya wakuu wa ujumbe wa uchumi wa China na Marekani yaliyofanyika kwa simu tarehe 5 mwezi huu, pande hizo mbili zimekubaliana kufanya Mazungumzo ya raundi ya 13 ya ngazi ya juu ya uchumi na biashara mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Kabla ya kufanyika kwa mazungumzo ya raundi hiyo, pande hizo mbili zimechukua hatua za kuonesha msimamo chanya, na kuchukua hatua za kusaidiana, ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuhimiza mazungumzo hayo kupata maendeleo yenye ufanisi, hali ambayo inalingana na matarajio ya jumuiya ya kimataifa. Mchakato wa mazungumzo hayo unaoendelea kwa mwaka mmoja umeonesha kuwa, hamna mshindi katika vita vya biashara, na kitendo cha kuendelea kuongeza ushuru wa bidhaa hakitasaidia kufumbua suala hilo. Bali kushikilia usawa na kuheshimiana, na kufanya mazungumzo na ushirikiano kwa msimamo wa kimantiki tu ndio zitaweza kusaidia kuondoa migogoro na mikwaruzano.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa nchi hizo mbili nchini Argentina na huko Osaka, ujumbe wa uchumi na biashara kati ya pande hizo mbili unatakiwa kuharakisha hatua ya kufanya mazungumzo ya kuelekea kuondoa ushuru ulioongezwa, ili kufikia mapema makubaliano halisi yatakayonufaisha pande zote mbili. Ili kutimiza lengo hilo, China na Marekani zinatakiwa kuimarisha maelewano, kuheshimu tofauti wakati wa kutafuta maslahi ya pamoja, na kutatua mikwaruzano kwa njia ya ushirikiano. Hili ni jukumu la pamoja kwa nchi hizo mbili kwa amani na maendeleo ya dunia.

China na Marekani yakiwa makundi makubwa ya kiuchumi duniani, zina maslahi mengi ya pamoja, na maendeleo makubwa ya ushirikiano. Tofauti zilizopo kati ya pande hizo mbili zinatakiwa kuondolewa kwa njia ya mazungumzo, na kutafuta njia za utatuzi zinazoweza kukubaliwa na pande hizo mbili. China inapinga kithabiti kupandisha ngazi ya vita vya biashara, ikizitaka pande hizo mbili ziendelee kufanya juhudi za kusaidiana, kufuata makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa nchi hizo mbili, kushikilia usawa na kuheshimiana, kuendelea kujizuiza, kuongeza maelewano, na kupanua maafikiano ya pamoja, ili kuhimiza kufikiwa kwa makubaliano ya uchumi na biashara ambayo yanaweza kukubaliwa na pande zote mbili na kunufaishana, hali ambayo itaisaidia China, Marekani hata dunia nzima.