China yatoa uzoefu mzuri kwa juhudi za kupunguza umaskini duniani
2019-10-04 18:10:54| CRI

Zaidi ya Wachina milioni 850 wameondolewa kwenye umaskini uliokithiri katika miongo saba iliyopita tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, na kati ya mwaka 2013 hadi 2018, kila mwaka zaidi ya watu milioni 12 waliondokana na umaskini nchini China. Shirika Kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri yenye kichwa cha "China yatoa uzoefu mzuri kwa juhudi za kupunguza umaskini duniani".

Wakati China ikiadhimisha miongo saba tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, mwanasayansi wa kilimo mwenye umri wa miaka 90 Yuan Longping alipewa "Nishani ya Jamhuri", kutokana na utafiti wake wa mpunga chotara ambao umetoa mchango mkubwa kwa usalama wa chakula nchini China na duniani. Wakati China mpya ilipoanzishwa, wachina walikabiliwa na baa kubwa la njaa. Baada ya kufanya juhudi kubwa, haswa kupata mafanikio ya teknolojia ya mpunga chotara, China iliondokana na baa hilo, na kufanikiwa kuwalisha wachina wanaochukua asilimia 20 ya watu wa dunia kwa asilimia 9 ya mashamba ya dunia. Wakati huohuo, China imepata mafanikio makubwa katika kuondoa umaskini uliokithiri, na kufuatia mpango uliowekwa na serikali, mwakani, kwa ujumla China itatimiza lengo la kuondokana na umaskini uliokithiri.

Ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani, China imeharakisha mchakato wa kupambana na umaskini duniani. Si kama tu China imetangulia kutimiza lengo la kuondoa umaskini lililowekwa na Umoja wa Mataifa, bali pia imetoa misaada kwa nchi za Asia, Afrika na Latin-Amerika. Katika miaka 70 iliyopita, China imetoa misaada ya dola za kimarekani zaidi ya bilioni 56.3 kwa nchi na mashirika 170, na kutuma watu zaidi ya laki sita kutekeleza miradi zaidi ya 5,000 ya misaada katika nchi za nje. Zaidi ya hayo, China imetoa ufadhili wa masomo kwa watu zaidi ya milioni mbili wanaotoka nchi zinazoendelea.

Njia na uzoefu wa China katika kuondoa umaskini vimetoa elimu na mpango wa kichina kwa ajili ya juhudi za kupambana na umaskini duniani. Kitabu cha "Kuondoa Umaskini" kilichoandikiwa na Rais Xi Jinping wa China kimefuatiliwa na nchi zinazoendelea. Maofisa wengi wa nchi za Afrika wanaona kuwa, kitabu hiki si kama tu ni kwa ajili ya wasomaji wa China, bali pia ni kwa ajili ya nchi na watu wote wanaotaka kuondoa umaskini duniani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema, mkakati wa China wa kupunguza umaskini kwa ubainishaji ni njia pekee ya kuwasaidia watu maskini na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.

Kutokana na athari za vitendo vya kupinga utandawazi wa uchumi, kutokuwepo kwa uwiano wa maendeleo na ugaidi, hadi sasa zaidi ya watu milioni 700 duniani wanakumbwa na umaskini uliokithiri. Ikiwa nchi kubwa inayowajibika na kuwa na uzoefu mkubwa wa kupunguza umaskini, China itaendelea kuzingatia ushirikiano wa kunufaishana, na kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea kuongeza uwezo wa kupata maendeleo endelevu kwa kuongeza kuagiza bidhaa na uwekezaji katika nchi hizo.

Takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia zinaonesha kuwa, pendekezo la China la "Ukanda Mmoja, Njia Moja" litazisaidia nchi husika kuondoa umaskini uliokithiri kwa watu milioni 7.6, na umaskini wa kiwango cha kati kwa watu milioni 32. Mwaka 2015, China ilianzisha Mfuko wa Msaada wa Ushirikiano kati ya Nchi za Kusini, na hadi mwaka jana, mfuko huo ulitekeleza miradi zaidi ya 200 katika nchi zaidi ya 30. Kwenye mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana mjini Beijing, China iliahidi kufanya ushirikiano na nchi za Afrika katika kuhimiza maendeleo ya viwanda, na ujenzi wa uwezo. Katika siku za baadaye, China pamoja na nchi nyingine zitaendelea kunufaika na uzoefu na matokeo yake ya kupunguza umaskini, na kutoa mchango kwa ajili ya kujenga uhusiano mpya wa ushirikiano na mawasiliano katika mapambano dhidi ya umaskini duniani.