China na Marekani zasuluhisha mvutano wa kibiashara kwa njia mwafaka
2019-10-15 19:38:02| CRI

Duru mpya ya mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya China na Marekani kuhusu suala la kibiashara imefanyika hivi karibuni mjini Washington, na kupiga hatua halisi katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, ulinzi wa hakimiliki za kiubunifu, kiwango cha ubadilishaji wa fedha, huduma za kifedha, kupanua ushirikiano wa kibiashara, utoaji wa teknolojia, na utatuzi wa migongano. Pande hizo mbili zitaendelea na mazungumzo hayo ili kufikia makubaliano ya mwisho.

Matokeo makubwa ya mazungumzo hayo ni kwamba, China na Marekani zimetafuta usuluhishi kwa busara ya juu ya kisiasa, kwani pande hizo mbili zimetambua kuwa kuzingatia maslahi ya wateja na wazalishaji, na kutafuta utatuzi kuanzia mambo yenye tofauti kidogo zaidi ni njia mwafaka zaidi.

Suala la biashara ni nanga ya kutuliza uhusiano kati ya China na Marekani, kushughulikia vizuri suala hilo kunanufaisha amani na ustawi wa China, Marekani na dunia nzima, na haya ni maoni mapya ya pamoja yaliyofikiwa na nchi hizo. Baada ya kupiga hatua, China na Marekani zinapaswa kuendelea na juhudi za pamoja, na kujitahidi kufikia makubaliano ya mwisho, ili kuhimiza uhusiano kati yao kuelekea njia sahihi.