China yaonesha imani ya kiuchumi kwa kufungua zaidi sekta ya fedha
2019-10-17 19:00:19| CRI

Serikali ya China imeamua kurekebisha sheria kuhusu usimamizi wake kwa makampuni ya nje ya bima na benki, ili kufungua mlango zaidi kwa sekta ya fedha, hatua inayoonesha imani ya China kuhusu uchumi wake, na pia italeta injini mpya kwa ukuaji wa uchumi wa dunia.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imefungua mlango katika sekta ya fedha hatua kwa hatua, haswa tangu rais Xi Jinping atangeze sera mpya kwenye Baraza la Bo'ao mwaka jana. Uamuzi wa kurekebisha sheria utarahisisha masharti ya benki na mashirika ya nchi za nje kuingia kwenye soko la China, na kuziwekea mazingira huru zaidi.

Sekta ya fedha ni nguzo ya uchumi, na kufungua mlango kwa sekta hiyo kunahitaji ujasiri mkubwa. Hivi sasa dunia inakabiliwa na ongezeko la vitendo vya kujilinda kibiashara, lakini uchumi wa China umedumisha maendeleo ya utulivu. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kasi ya ongezeko la uchumi wa China ilifikia asilimia 6.3 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hiki. Ripoti ya mwaka 2019 ya ushindani ya kiuchumi duniani iliyotolewa na Baraza la Uchumi wa Dunia imeipa China alama ya 98.8 kutokana na utulivu wa uchumi.

Aidha, kufuatia mageuzi ya sekta ya fedha na ongezeko la ushindani wa sekta hiyo nchini China, maendeleo ya uchumi wa dunia pia yatapata injini mpya.