Uchumi wa China waendelea kwa utulivu ingawa unakabiliwa na changamoto
2019-10-18 18:57:53| CRI

Takwimu zilizotolewa leo na Idara Kuu ya Takwimu ya China zinaonesha kuwa, katika robo tatu za mwanzo mwaka huu, pato la taifa la China GDP limezidi dola za kimarekani trilioni 9.87, na kuongezeka kwa asilimia 6.2 ikilinganishwa na mwaka jana kipindi kama hiki.

Msemaji wa Idara Kuu ya Takwimu ya China Bw. Mao Shengyong amesema, katika kipindi hicho, uchumi wa China umeendelea kwa utulivu, muundo wake umeboreshwa, huku kiwango cha maisha ya watu kikiinuka kwa mfululizo.

Kutokana na ongezeko la vitendo vya upande mmoja na vitendo vya kujilinda kibiashara, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia na biashara ya kimataifa imepungua. Hata hivyo China imedumisha hali nzuri ya maendeleo ya uchumi. Sababu muhimu ni kwamba, China imetekeleza sera chanya za kiuchumi, ikiwemo sera mwafaka ya kifedha, na kupunguza ushuru, wakati huo huo, China pia imefungua mlango zaidi ili kuhimiza uboreshaji wa muundo wa uchumi.

Hali ya utulivu ya maendeleo ya uchumi pia inatokana na juhudi za makampuni. Katika kipindi hiki muhimu, makampuni ya China yameongeza uwekezaji katika uvumbuzi ili kukuza nguvu ya ushindani.

Tangu mwaka 2006, China imeshika nafasi ya kwanza kwa kutoa mchango zaidi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa miaka 13 mfululizo. Wakati uchumi wa dunia unapokabiliwa na changamoto, China itaendelea kuwa injini muhimu ya ongezeko la uchumi huo.