Tarehe 11 Novemba ni "Siku ya Manunuzi" ambayo iliwadia siku moja baada ya Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Uingizaji wa Bidhaa za Nje ya China. Katika siku hiyo, thamani ya mauzo ya bidhaa kupitia Taobao na Jingdong ambayo ni makampuni makubwa ya mauzo kupitia mtandao wa Internet nchini China ilizidi dola bilioni 38.3 na 29.2 za kimarekani. Shirika kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri yenye kichwa cha habari "Mauzo mazuri ya Siku ya Manunuzi ya Novemba 11 yathibitisha uhai mkubwa wa uchumi wa China.
Huu ni mwaka wa 11 tangu China kuanzisha "Siku ya Manunuzi ya Novemba 11", na China inaharakisha kuinua kiwango cha matumizi ya wateja. Hivi sasa wateja wa China wanapendelea bidhaa zenye ubora na teknolojia ya juu na kuweza kukidhi mahitaji yao maalumu, na simu ya mkononi imekuwa zana yao kuu ya kufanya manunuzi.
Katika siku hiyo ya mwaka huu, makampuni mengi ya mauzo kupitia mtandao wa Internet yamezingatia soko la miji midogo na vijiji, kwani asilimia 70 ya wateja wanatoka sehemu hizo. Takwimu zinaonesha kuwa ongezeko la thamani ya mauzo ya baadhi ya bidhaa katika sehemu hizo limezidi asilimia 100, na soko linaloibuka la sehemu hizo limekuwa injini muhimu ya maendeleo ya uchumi wa China.
Katika siku hiyo ya mwaka huu, makampuni ya mauzo kupitia mtandao wa Internet yametoa bidhaa nyingi mpya. Kwa mfano tovuti ya Tianmao ya Taobao ilitoa bidhaa milioni moja mpya, huku asilimia 90 ya bidhaa ndogo zikichagua Jingdong kuwa jukwaa la kwanza la kuuzwa. Hali hii inaonesha kuwa makampuni ya China yameongeza uwekezaji katika utafiti wa matoleo mapya.
Bidhaa za nchi za nje pia zimependwa na wateja wa China katika siku hiyo. Katika Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Uingizaji wa Bidhaa za nje ya China, thamani ya makubaliano ya maagizo ya bidhaa ilizidi dola bilioni 71.13. Bidhaa za nje zinazopendwa zaidi na wachina ni pamoja na mapambo, vitu vya kitamaduni na chakula maalumu. Mwaka huu makampuni ya nchi za nje yaliyojiandikisha kwenye tovuti ya mauzo ya Tianmao ya Taobao yameongezeka kwa asilimia 300, na kati ya makampuni hayo, mengi yanatoka Marekani, Uingereza na Japan. Hali hii inaonesha kuwa kauli ya "kutengana kwa masoko ya magharibi na China" haina msingi wowote.
Matumizi ni nguzo ya kimsingi ya maendeleo ya uchumi. Kutokana na idadi kubwa ya watu, ongezeko la mapato ya wananchi, na matumaini ya kuboresha maisha ya watu, China ina soko kubwa mno, ambalo limekuwa injini muhimu ya maendeleo yenye sifa zaidi ya uchumi wa China. Katika robo tatu za mwanzo ya mwaka huu, mchango wa matumizi kwa maendeleo ya uchumi umefikia asilimia 60.5. Wakati China inapokabiliwa na changamoto ya ongezeko la vitendo vya kujilinda kibiashara, na kudidimia kwa uchumi wa dunia, mauzo ya "Siku ya Manunuzi ya Novemba 11" yanaonesha kuwa, soko linaloibuka la ndani ni msingi imara wa ukuaji wa uchumi.