China haitashindwa na tishio lolote la nje
2019-11-29 18:46:19| CRI

Serikali ya Marekani hivi karibuni imesaini "Mswada wa Haki za Binadamu na Demokrasia ya Hong Kong" na kuuidhinisha kuwa sheria, ili kuunga mkono watu wenye msimamo mkali wanaovuruga utulivu mkoani Hong Kong. Kitendo hicho kimeingilia kati mambo ya Hong Kong, ambayo ni mambo ya ndani ya China, na kukiuka sheria ya kimataifa na kanuni ya kimsingi ya uhusiano wa kimataifa. Shirika Kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri inayosema China haitashindwa na tishio lolote la nje.

Tahariri hiyo inasema, katika miezi mitano iliyopita, vurugu za kimabavu zimezidi kupamba moto mkoani Hong Kong, na kuuletea mkoa huo wenye utawala maalumu wa China hatari kubwa. Waandamanaji wakipaza sauti za "uhuru wa Hong Kong" wamefunga barabara, kuchoma moto, kushambulia polisi, raia wa kawaida, na wazalendo wanaowapinga, na kusababisha kifo cha mtu mmoja. Wakati huohuo, Marekani imepitisha "Mswada wa Haki za Binadamu na Demokrasia ya Hong Kong" ili kuunga mkono waandamanaji hao, kwa hila ya kuharibu ustawi na utulivu wa Hong Kong, na kuzuia maendeleo ya China.

Kwa miaka mingi iliyopita, mara kwa mara Marekani imeingilia kati mambo ya Hong Kong, na kujaribu kuvurugu mkoa huo ili kujipatia maslahi. Katika miaka 30 kati ya mwaka 1984 na 2014, Marekani ilitoa miswada zaidi ya 40 kuhusu mambo ya Hong Kong. Mwaka 2014 mashirika kadhaa ya Marekani ikiwemo Mfuko wa Kitaifa wa Demokrasia ya nchi hiyo, yalitoa misaada ya fedha kwa watu walioandamana kwenye uwanja wa Zhonghuan mkoani Hong Kong. Mwaka huu, wanasiasi kadhaa wa Marekani walikutana na viongozi wa watu wanaodai "Hong Kong kujitenga na China". Wakati huohuo, vyombo vya habari vya Marekani vimepotosha ukweli, na kuunga mkono waandamanaji wanaofanya vurugu.

Wachina wana desturi ya kutoshindwa na matishio ya nje. Wakati Jamhuri ya Watu wa China ilipoasisiwa, iliwekewa vikwazo na nchi za magharibi haswa Marekani. Wakati huo, ingawa walikuwa wakikabiliwa na taabu kubwa, lakini Wachina hawakushindwa hata kidogo. Tangu Hong Kong kurudishwa China, kutokana na uungaji mkono wenye nguvu kubwa kutoka serikali kuu, mkoa huo umedumisha utulivu na ustawi wa muda mrefu. Marekani haitawatishia Wachina kwa kupitisha "Mswada wa Haki za Binadamu na Demokrasia ya Hong Kong", kwani wana nia thabiti ya kulinda ustawi na utulivu wa Hong Kong, na mamalaka, usalama na maslahi ya kimaendeleo ya taifa la China. Hivyo mswada huo unaweza tu kuwafahamisha Wachina kuhusu umwamba na hila ya Marekani, na kuwafanya washikamane zaidi ili kukabiliana na matishio ya nje.

Hong Kong ni sehemu ya China, na nchi yoyote ya nje hairuhusiwi kuingilia kati mambo yake. Hivi sasa China ina nguvu kubwa zaidi kuliko zamani katika kukabiliana na changamoto za nje. Jambo ambalo Marekani inapaswa kufanya, ni kusimamisha mara moja vitendo vya kuingilia kati mambo ya Hong Kong na mambo mengine ya ndani ya China.