China yasikitishwa na kukwama kwa idara ya kusikiliza mastaka ya WTO
2019-12-12 19:59:32| CRI

Msemaji wa wizara ya biashara ya China Bw. Gao Feng amesema, hivi sasa idara ya kushughulikia mashtaka iliyo chini ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) imesimamishwa, na hili ni pigo kubwa zaidi kwa Shirika hilo tangu lianzishwe.

Bw. Gao amesisitiza kuwa, China inaona idara hiyo ni muhimu sana kwa kudumisha utulivu, mamlaka na ufanisi wa WTO, na utaratibu wa pande nyingi wa kibiashara duniani, hivyo inaunga mkono pande mbalimbali kufanya juhudi ili kurejesha kazi za idara hiyo.

Shirika Kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri yenye kichwa cha "changamoto ya WTO yadhihirisha umuhimu wa kupinga kithabiti vitendo vya kujilinda kibiashara na vitendo vya upande mmoja", ikiwa ni kuhusiana na kusimamishwa kwa Idara ya Kushughulikia Mashtaka ya WTO. Tahariri hiyo inasema, katika miaka 25 iliyopita tangu WTO ianzishwe, idara hiyo imetoa hukumu kwa kesi zaidi ya 200, na kutatua mivutano mingi ya kibiashara. Lakini tangu awamu hii ya serikali ya Marekani iwe madarakani, imezuia uteuzi wa majaji ya idara hiyo, na hadi sasa idara hiyo iliyokuwa na majaji saba ina jaji mmoja tu, na haiwezi kuendelea na kazi tena. Kitendo hicho kimeonesha umwamba wa Marekani, na kulaumiwa vikali na jumuiya ya kimataifa.

Ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea, na nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi, China inalinda kithabiti biashara huria na utaratibu wa biashara wa pande nyingi, na itashirikiana na nchi nyingine kukabiliana na changamoto inayokabili WTO.