China ina uwezo wa kushinda changamoto za kiuchumi
2019-12-13 18:59:22| CRI

Mkutano wa siku tatu wa kazi za kiuchumi wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China umefungwa, baada ya kujadili kazi za kiuchumi za mwaka huu, kuchunguza hali ya uchumi ya hivi sasa, na kupanga kazi za kiuchumi za mwakani. Shirika Kuu la Utangazaji la China limetoa tahariri kuhusu mkutano huo inayoitwa "China ina uwezo wa kutosha kushinda changamoto za kiuchumi"

Tahariri hiyo inasema, mkutano wa kazi za kiuchumi wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China ni dirisha muhimu la kuangalia mpangilio wa sera za kiuchumi za China katika mwaka ujao. Mwaka 2020 ni mwaka wa mwisho wa China kujenga jamii yenye maisha bora na mpango wa 13 wa miaka mitano, licha ya hayo, China inakabiliwa na hali tete ya ndani na ya nje, hivyo mkutano huo umefuatiliwa sana.

Kutokana na mkutano huo, hivi sasa uchumi wa China unakabiliwa na changamoto mbalimbali za ndani na nje, lakini kwa upande mwingine, mwelekeo wa ukuaji mzuri haujabadilika, na kutokana na kuwa na mfumo maalumu wa kisiasa, rasilimali kubwa zilizolimbikizwa tangu kuanzishwa kwa sera ya mageuzi na kufungua mlango, soko kubwa, na nguvukazi kubwa, China itashinda changamoto yoyote inayoikabili.

Mkutano huo umesisitiza kuwa, ili kutimiza lengo la ukuaji wa uchumi mwakani, China itadumisha sera tulivu, na kufanya kazi sita muhimu, ambazo ni kutekeleza mawazo mapya ya maendeleo kwa nia thabiti, kushughulikia vizuri masuala matatu muhimu ya kukinga matishio makubwa, kuondoa umaskini na kuhifadhi mazingira, kuhakikisha maisha ya watu haswa wale maskini, kuendelea kutekeleza sera chanya za kifedha, kuhimiza maendeleo yenye sifa ya juu na kusukuma mbele mageuzi ya uchumi.

Kuhusu suala la kuondoa umaskini ambalo linafuatiliwa zaidi, mkutano huo umesema China itakusanya nguvu kutokomeza umaskini uliokithiri, kutekeleza kiuhalisi hatua za kuondoa umaskini kupitia kuendeleza sekta za uchumi, na kuwahamisha watu maskini kutoka sehemu zenye mazingira magumu ya kimaisha.

Aidha, mkutano huo umesisitiza kuwa, China itaendelea na mageuzi katika nyanja nyingi zaidi na kwa kina zaidi, ikiwemo kuhimiza na kulinda uwekezaji wa nje, kupunguza sekta wawekezaji wa nje wanazopigwa marufuku kuingia, kuhamasisha makampuni ya ndani kupanua masoko ya nje, kupunguza zaidi kiwango cha ushuru, kukamilisha mfumo wa sera na huduma za uwekezaji wa "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na kuharakisha mazungumzo kuhusu biashara huria ya pande mbili na pande nyingi.

Katika miaka 70 iliyopita tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, uchumi wa China umekua baada ya kushinda changamoto moja baada ya nyingine. Endapo China itatumia vizuri rasilimali zake za mfumo wa kisiasa, soko na nguvukazi, uchumi wake utakuwa na maendeleo ya sifa nzuri zaidi, na kutoa mchango mkubwa zaidi kwa ajili ya ustawi na maendeleo duniani.