China yajitahidi kusonga mbele kwa pamoja na dunia nzima
2020-01-01 16:50:30| CRI

Wakati mwaka 2020 ulipokaribia, rais Xi Jinping wa China alitoa salamu za mwaka mpya kupitia Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG na mtandao wa Internet, kuhitimisha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka uliopita, na kuangalia mustakabali wa maendeleo katika mwaka 2020.

Katika hotuba hiyo, rais Xi alisema mwaka 2019 ulikuwa mwaka usio wa kawaida kwa China na dunia. Mwaka huo, vitendo vya upande mmoja na kujilinda kibiashara viliibuka, mikwaruzano ya kibiashara iliongezeka, na makundi mbalimbali ya kiuchumi duniani yalikabiliwa na mashinikizo mbalimbali ya maendeleo. Mwaka huo pia ulikuwa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuasisiwa kwa China mpya, pato la ndani la taifa linakadiriwa kukaribia dola za kimarekani trilioni 14, huku wastani wa kila mtu ukifikia dola za kimarekani elfu kumi. Takwimu hizo zimeonesha kuwa, China inaelekea kuwa nchi yenye pato la kiwango cha juu duniani, hali ambayo itahimiza kuongezeka kwa uwezo na mahitaji ya matumizi ya wachina, na kufungua soko kubwa zaidi kwa dunia.

Maendeleo yaliyopatikana na China katika mwaka 2019 yalionesha sura na nguvu ya China kwa dunia, ambayo yanategemea mageuzi, ufunguaji mlango na uvumbuzi. Pia yameonesha kuwa China imekuwa ikisukuma mbele maendeleo yenye ubora wa hali ya juu, na kuthibitisha kuwa imetekeleza ahadi yake ya kufanya mageuzi na ufunguaji mlango.

Wakati huo huo, China inazikaribisha nchi mbalimbali kupanda kwa pamoja "gari" la maendeleo la China. Mwaka 2019, makubaliano 283 yalifikiwa kwenye Mkutano wa pili wa kilele wa Baraza la Ushirikiano wa Kimataifa la "Ukanda Mmoja, Njia Moja", thamani ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye Maonesho ya pili ya CIIE yenye kiwango cha juu cha sayansi na teknolojia ilifikia dola za kimarekani bilioni 64, na idadi ya nchi zilizoanzisha uhusiano wa kibalozi na China ilifikia 180, hali hii ni uungaji mkono mkubwa wa jumuiya ya kimataifa kwa mchango wa China.

Lengo la kuhitimisha maendeleo yaliyopatikana ni kupata maendeleo mapya katika siku za baadaye. Mwaka 2020 ni mwaka muhimu katika historia, ambapo China itakamilisha kwa pande zote ujenzi wa jamii yenye maisha bora, na kutimiza lengo la maendeleo la "Miaka 100 ya Kwanza". Mwaka 2020 pia utakuwa ni mwaka wa kunyakua ushindi wa mwisho kwenye mapambano magumu ya kutokomeza umaskini.

Mwaka 2020, China itaendelea kushikilia kanuni za amani, ufunguaji mlango na maendeleo, kushirikiana na nchi mbalimbali kujenga kwa pamoja "Ukanda Mmoja, Njia Moja", na kuhimiza kujenga Jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja. Hizi ni chaguo na mahitaji ya China katika kujiendeleza, vilevile ni ahadi iliyoitoa China kwa dunia katika mwaka mpya.