Makubaliano ya kunufaishana kati ya China na Marekani kuhimiza amani na utulivu duniani
2020-01-16 09:51:21| CRI

China na Marekani zimesaini makubaliano ya awali kuhusu suala la uchumi na biashara. Kwenye hafla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, mwakilishi wa China ambaye pia ni naibu waziri mkuu wa China Bw. Liu He amesema, makubaliano hayo yatanufaisha China, Marekani na dunia nzima. Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG limetoa tahariri ya "Makubaliano ya kunufaishana kati ya China na Marekani kuhimiza amani na utulivu duniani".

Tahariri hiyo inasema ilikuwa vigumu kwa China na Marekani kufikia makubaliano kuhusu suala la uchumi na biashara, kwani zimefanya duru 13 za mazungumzo katika miezi 23 iliyopita. Makubaliano hayo yana vipengele tisa, ikiwa ni pamoja na hakimiliki za ubunifu, utoaji wa teknolojia, chakula na mazao ya kilimo, huduma za kifedha, kiwango cha ubadilishaji wa fedha, kupanua biashara, utaratibu wa tathmini ya pamoja na utatuzi wa mivutano.

Tahariri hiyo inaona kuwa maonesho hayo yameonesha usawa na uwiano. Kwa mfano, kipengele cha hakimiliki za ubunifu kimehusisha pande zote za ulinzi wa hakimiliki za ubunifu duniani, na si kama tu kitasaidia China kujijenga kuwa nchi inayozingatia zaidi uvumbuzi, kuendeleza makampuni ya uvumbuzi, na kulinda maslahi halali ya makampuni mbalimbali yakiwemo ya nchi za nje, bali pia kitalinda maslahi ya makampuni ya China zinazofanya biashara nchini Marekani. Makubaliano hayo pia yatatimiza hali ya kunufaishana na kupata mafanikio ya pamoja, hali ambayo ni kiini cha ushirikiano wa uchumi na biashara kati ya China na Marekani. Kwa mfano, kipengele cha chakula na mazao ya kilimo kinahusisha maziwa, nyama ya kuku, nyama ya ng'ombe, nyama ya nguruwe, nyama za kusindikwa, samaki, mchele, matunda, chakula cha mifugo na chakula cha wanyama kipenzi, na hizo ndio bidhaa zinazohitajika zaidi kwa wateja wa China. China ni nchi inayoagiza zaidi mazao ya kilimo, huku Marekani ikiwa nchi inayouza zaidi mazao hayo, na kuongeza ushirikiano katika sekta ya kilimo kutanufaisha nchi hizo zote.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, China itaongeza ushirikiano wa kibiashara na Marekani, kupunguza sekta za soko zinazopiga marufuku kampuni za nje, na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara. Hali hii inaendana na mahitaji ya maendeleo ya sifa ya juu ya China, na pia itakidhi matakwa ya Marekani.

Hivi sasa dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika miaka 100 iliyopita, na sintofahamu za maendeleo ya uchumi wa dunia zinaongezeka. China na Marekani ni nchi zenye nguvu zaidi ya kiuchumi duniani, uhusiano kati yao katika uchumi na biashara ni nguzo ya kutuliza uchumi wa dunia. Makubaliano ya kipindi cha kwanza ya uchumi na biashara kati ya nchi hizo yatapunguza hali ya wasiwasi ya biashara duniani, na kuleta utulivu kwa maendeleo ya dunia.