Tahariri: Rais wa China kutumia barua mbili Afrika ndani ya wiki moja kunaleta ishara gani?
2020-02-11 18:22:15| CRI

Tarehe 9, Februari, rais Xi Jinping wa China alituma barua kwa mkutano wa 33 wa wakuu wa Umoja wa Afrika ulioanza Addis Ababa, Ethiopia akipongeza nchi za Afrika na watu wake. Kabla ya hapo tarehe 2, Februari, rais Xi pia alimtumia barua rais Macky Sall wa Senegal ambayo ni nchi mwenyekiti mwenza wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC akipongeza miaka 20 tangu kuanzishwa kwa FOCAC. Ndani ya wiki moja tu rais Xi alitumia barua mbili Afrika, jambo ambalo limetoa ishara zifuatazo: uhusiano kati ya China na Afrika uko katika kipindi kizuri zaidi cha kihistoria, China na Afrika zinajitahidi kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati yao iliyo na uhusiano wa karibu zaidi, na pia kuonesha urafiki wa dhati kati ya China na Afrika wakati China inakabiliwa na kipindi kigumu cha maambukizi ya virusi vipya vya korona.

Urafiki kati ya China na Afrika ni wa muda mrefu na umehimili changamoto mbalimbali za kihistoria, na umekuwa mfano wa kuigwa katika ushirikiano kati ya Kusini na Kusini. Utamaduni wa jadi wa waziri wa mambo ya nje wa China kufanya ziara yake ya kwanza mwanzoni mwa kila mwaka katika nchi za Afrika umedumu kwa miaka 30. Miradi mbalimbali inayofadhiliwa na China barani Afrika kama vile reli ya TAZARA na jengo la mkutano wa Umoja wa Afrika pia ni ushahidi wa kihistoria na kumbukumbu nzuri ya urafiki kati ya China na Afrika. Mwezi Septemba mwaka 2018, mkutano wa kilele FOCAC ulifanyika mjini Beijing, na ulitoa mpango na maelekezo mapya kuhusu jinsi ya kukuza zaidi uhusiano kati ya China na Afrika, na maendeleo mapya ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili yamepatikana katika miaka inayofuata.

China na Afrika pia zimekabiliwa kwa pamoja na changamoto mbalimbali na hatma zao zimejengwa kuwa za pamoja katika mchakato huo. Mwaka 2014, nchi kadhaa za Afrika Magharibi ikiwemo Senegal zilipatwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Wakati nchi za magharibi zilipowaondoa raia wao, China ilikuwa nchi ya kwanza kukodi ndege kupeleka vitu vya uokoaji vya dharura na kutuma vikosi vya matibabu kusaidia kupambana na ugonjwa huo. Madaktari na wauguzi 1,200 ambao hawakujali hatari ya kuambukizwa virusi hivyo walikuwa mstari wa mbele katika vita hiyo.

Waswahili husema, Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Tangu mapema mwaka huu, China imekumbwa na maambukizi ya virusi vipya vya korona vinavyosababisha ugonjwa wa nimonia. Viongozi na wananchi wa nchi mbalimbali za Afrika wameeleza imani zao kwa juhudi za China za kupambana na maambukizi hayo. Tarehe 9, Februari katika mkutano wa 33 wa wakuu wa Umoja wa Afrika, washiriki mbalimbali wameeleza kuunga mkono juhudi za China. Baraza la utendaji la Umoja wa Afrika limetoa taarifa likisema mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja huo wamepongeza juhudi za serikali ya China na wananchi wake katika mapambano dhidi ya virusi vipya vya korona, na kusema wana imani na uwezo wa serikali hiyo katika mapambano hayo. Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, amesema katika kipindi hiki muhimu, Afrika iko pamoja na marafiki wa kichina wanaoathiriwa na maambukizi ya virusi vipya vya korona. Naye mwenyekiti wa kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mohamed Bandi, amesema serikali ya China imetoa taarifa kuhusiana na maambukizi hayo kwa uwazi na wakati, na amepongeza kazi zinazofanywa na China katika kuzuia na kudhibiti maambukizi hayo.

Maambukizi ya virusi ni ya muda mfupi, lakini urafiki unadumu kwa muda mrefu. Kama alivyosema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Geng Shuang, baada ya taabu ya maambukizi hayo, urafiki kati ya watu wa China na Afrika utaimarishwa zaidi na jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Afrika itakuwa imara zaidi.