Mfadhaiko wa Pelosi waonesha kukosa kwa hadhi ya nchi za magharibi
2020-02-16 18:32:52| CRI

Kwenye mkutano wa usalama wa Munich uliofanyika juzi, spika wa baraza la chini la bunge la Marekani Bi Nancy Pelosi ameilaumu China kujaribu kueneza "udikteta wa kidigitali" kupitia kampuni ya teknolojia ya juu ya Huawei, huku akidai kuwa China inatishia kuzilipizia kisasi nchi zisizotumia teknolojia za Huawei. Mwanadiplomasia wa China Bi Fu Ying akijibu hoja hiyo alisema, tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango katika miaka arobaini iliyopita, China imeingiza teknolojia mbalimbali kutoka nchi za magharibi, kampuni zikiwemo Microsoft, IBM na Amazon zote zinafanya shughuli zao nchini China. Anaona teknolojia hizo hazikutishia mfumo wa kisiasa wa China, bali zimeisaidia China kupata maendeleo makubwa. Aliendelea na kuuliza, "ni vipi kuingiza teknolojia ya mtandao wa 5G ya Huawei katika nchi za Magharibi, kutatishia mfumo wa kisiasa wa nchi hizo? Je mfumo wa kidemokrasia ni dhaifu sana kiasi cha kutishiwa na kampuni ya teknolojia ya juu ya Huawei?" Swali la Bi Fu Ying lilipigiwa makofi na washiriki wa mkutano huo, Bi Pelosi alionekana kufadhaika akidai kuwa kampuni za China ikiwemo Huawei si za mtindo wa kampuni huria. Lakini je marafiki wa Bi Pelosi kutoka Ulaya pia anaona hivyo? Jibu ni hapana.   

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi aliyehudhuria mkutano huo amesema, nchi nyingi ikiwemo Uingereza na Ujerumani haziamini uvumi, na zinapenda kutoa mazingira yenye ushindani wa usawa kwa kampuni za nchi mbalimbali kwa msingi wa kulinda usalama wa miundombinu ya mawasiliano ya habari. Kwa nini Marekani haiwezi kukubali kampuni za nchi nyingine kujitokeza kwenye sekta za uchumi na teknolojia? Sababu ni kwamba haitaki kuona nchi nyingine kujipatia maendeleo na kampuni za nchi nyingine kujiendeleza.

Kanuni ya kutobagua ni moja ya kanuni muhimu za uchumi wa soko huria, yaani "mtindo wa kampuni huria" kama alivyosema Bi Pelosi, ambayo ni makubaliano makini kuhusu ushindani wenye usawa uliofikiwa na pande mbalimbali wa sokoni. Lakini baadhi ya wanasiasa wa Marekani sio tu wameharibu makubaliano hayo katika suala la Huawei, bali pia wanafanya chini juu kuzuia wenzi wa Ulaya kushirikiana na kampuni ya Huawei.

Kimsingi, teknolojia ya mtandao wa 5G ya Huawei si changamoto kwa demokrasia ya kimagharibi, lakini changamoto zimetokea ndani ya nchi za magharibi. Karibuni tu, kitendo cha Bi Pelosi kuchana hotuba ya rais bungeni kilionesha hali ya mgawanyo kwa vyama viwili vya kisiasa vya Marekani na msimamo mkali wa siasa. Kuongezeka kwa msimamo mkali wa kisiasa kumeifanya demokrasia ya kimagharibi iwe dhaifu zaidi, na kuufanya uchaguzi kuwa faraja kwa umma na kuhimiza harakati ya kupinga utandawazi duniani. Kampuni ya Huawei imekuwa ni mhanga wa hali hiyo.

Kaulimbiu ya mkutano huo wa usalama ni kukosa wa magharibi. Kama alivyosema mwenyekiti wa mkutano huo Bw. Wolfgang Ischinger, hivi sasa nchi za magharibi si za magharibi kama ilivyokuwa zamani, na dunia si ya magharibi kama ilivyokuwa zamani. Nyuma ya hali hiyo ni kiburi na hatua ya upande mmoja ya Marekani katika masuala mengi, ambayo imezidisha hali ya wasiwasi barani Ulaya.

Kuibuka kwa nchi zinazojitokeza kiuchumi ni moja ya hali za siasa ya kimataifa inayoikabili nchi za magharibi katika nusu ya kwanza ya karne 21. Hali hii itasaidia kuleta hali ya uwiano katika uhusiano kati ya nchi za Kusini na Kaskazini, na kuhimiza demokrasia katika uhusiano wa kimataifa.

Nchi za Ulaya zinatakiwa kushirikiana na nchi zinazojitokeza kiuchumi, na kuondokana na nadharia ya "Nchi za Magharibi kuwa Kiini cha Dunia".