Nia ya baadhi ya watu kutaka kuitenganisha China na pande nyingine imeshindwa
2020-02-17 21:10:49| CRI

Matukio mawili yametokea jana nchini China. La kwanza ni kwamba kikundi cha wataalamu kilichotumwa na Shirika la Afya Duniani WHO kimewasili Bejing, na la pili ni kuwa reli ya China na Ulaya inayobeba kontena 41 za mizigo imeondoka mji wa Zhengzhou, Henan na kuelekea Asia ya Kati, ikimaanisha reli hiyo imerejea rasmi katika hali ya kawaida. Matukio hayo mawili sio tu yanalenga kulinda maslahi ya wananchi wa China, bali pia yanalenga kulinda maslahi ya dunia nzima, pia yameonesha kuwa nia ya baadhi ya watu kutaka kuitenganisha China na pande nyingine imeshindwa.

Takwimu mpya zinaonesha kuwa, mpaka kufikia jana, idadi ya wagonjwa wapya wa COVID-19 katika sehemu mbalimbali za China bara isipokuwa mkoa wa Hubei imefikia 115, ambayo imepungua kwa siku 13 mfululizo. Hivi sasa, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuambukiziwa virusi hivyo nje ya China hakijafikia asilimia 1 ya wagonjwa wote. Kama mkurugenzi mkuu wa WHO Bw. Tedros Adhanom Ghebreyesus alivyosema, China imelipa gharama kubwa kuzuia kuenea kwa COVID-19 kutoka kwa chanzo chake, na kutoa nafasi kwa dunia kufanya maandalizi kukabiliana na maambukizi hayo. Lakini baadhi ya vyombo vya habari na wanasiasa wa magharibi wameendelea kutoa habari zisizo za kweli na kutaka kuitenganisha China na pande nyingine. Katika zama ya utandawazi, hakuna hoja yoyote inayoshangaza zaidi kuliko wazo la kuitenganisha China na nje.