Gazeti la The Wall Street Journal la Marekani limekosolewa na jumuiya ya kimataifa baada ya kutoa makala yenye ubaguzi dhidi ya wachina. Wafanyakazi 53 wa gazeti hilo wameuandikia barua ya pamoja uongozi wa gazeti hilo, wakilitaka liombe radhi kwa watu ambao hawakupendezwa na makala hiyo iliyoitwa "China ni wagonjwa wa kweli wa Asia".
Kama tujuavyo, kuna watu wa rangi mbalimbali wanaoishi nchini Marekani, na ubaguzi sio tu ni kosa la kisiasa, bali pia ni mwiko wa kimaadili, na pia ukiukwaji wa kanuni ya mienendo inayotambuliwa kimataifa. Lakini ili kuvutia wasomaji, gazeti la The Wall Street Journal lilitumia kichwa cha habari cha ubaguzi, kukiuka maadili ya kitaaluma, kuacha kanuni za kutoa ripoti zinazotetewa na gazeti hilo ambazo ni za kweli, haki na usahihi, na hata kupoteza moyo wa huruma na ubinadamu.
Hata hivyo, gazeti hilo lilikataa kuomba msamaha kwa kisingizio cha uhuru wa kutoa habari na tahariri baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa serikali ya China, na maelfu ya wachina waishio Marekani wakitoa wito kwa Ikulu ya Marekani kulilazimisha gazeti hilo liombe radhi.
China haiwezi kukaa kimya tu wakati inapochafuliwa kwa jina. Hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya China iliwafutia wanahabari watatu wa gazeti la The Wall Street Journal vibali vya kufanya kazi, ikiwa ni jibu dhidi ya gazeti hilo. Kinashangaza ni kuwa, akizungumzia hatua hiyo ya China ya kulinda maslahi yake, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo aliikosoa kwa kudai kuwa ni kukiuka "uhuru wa kutoa maoni".
Sasa barua pepe ya pamoja iliyoandikwa na wafanyakazi 53 wa gazeti hilo ni ushahidi kuwa jambo hilo halihusiani na uhuru wa kutoa maoni kama alivyodai Pompeo, wala sio suala la habari, bali ni ubaguzi wa rangi.
Katika kipindi muhimu cha kupambana na maambukizi ya virusi vya korona COVID-19, kitendo kilichofanywa na gazeti la The Wall Street Journal kimetoa ishara ya hatari kuwa, kwa Marekani na nchi nyingine za magharibi, kauli na vitendo vya ubaguzi dhidi ya China na watu wake vinarudia tena. Jambo ambalo sio tu linazuia juhudi za kupambana na maambukizi ya virusi vya korona kimataifa, bali pia litaweza kuharibu amani na maendeleo ya dunia.