Jopo la WHO lapongeza juhudi kubwa za China kukabiliana na COVID-19
2020-03-01 19:32:38| CRI

"China imechukua hatua za kukinga na kudhibiti maambukizi ya COVID19 kwa ujasiri zaidi, unyumbufu zaidi na wa kujituma zaidi katika historia"

Sentensi hiyo imo kwenye ripoti iliyotolewa Jumamosi na timu ya wataalam wa China na Shirika la Afya Duniani WHO kuhusu ugonjwa wa nimonia inayosababishwa na virusi vipya ya korona COVID-19 iliyomaliza ziara ya utafiti ya siku tisa nchini China. Mshauri mwandamizi wa mkurugenzi mkuu wa WHO Bw. Bruce Aylward ni kiongozi wa timu hiyo upande wa nchi za nje. Akizungumzia ziara hiyo na waandishi wa habari, Bw. Aylward alisema "nikiambukizwa virusi, ningependa kutibiwa China, na mbinu inayotumiwa na China ni njia pekee inayofahamika na kuthibitishwa kuwa na ufanisi na kwamba nchi nyingine zinapaswa kujifunza mfumo wa kitaaluma wa China wa kukabiliana na maambukizi hayo."

Ili kuokoa maisha ya watu, mchango mkubwa uliotolewa na China katika vifaa vya matibabu pia umetambuliwa na jopo hilo la wataalam. Bw. Aylward aliwaambia wanahabari kuwa "mimi niliwauliza wana mashine ngapi ya kusaidia kupumua, walinijibu kuna 50 hadi 60. Wana mashine ngapi ya mapafu bandia ECMO. Walijibu tano. Hospitali moja ina ECMO tano, hata hospitali za Ulaya hazina."

Kutokana na juhudi kubwa za China, hali ya maambukizi imetulia na kuboreka. Takwimu zimeonesha kuwa Jumamosi kulikuwa na maambukizi mapya matatu nje ya mkoa wa Hubei katika China bara, na idadi ambayo imekuwa tarakimu moja kwa siku tatu mfululizo.

Hata hivyo maambukizi yanaenea kwa kasi nje ya China. Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amepandisha ngazi ya tishio la COVID-19 kutoka "juu" ya awali hadi "juu sana". Namna ya kudhibiti maambukizi hayo duniani imekuwa jukumu la kwanza kwa jamii ya kimataifa.